The House of Favourite Newspapers

Tabia Zimewakosesha Wengi Mafanikio, Usiwe Miongoni Mwao!

NI ukweli ulio wazi kwamba, maisha yanahitaji uyakabili kwa kujitoa mzimamzima bila kujaribu wala kuingia nusunusu. Ni vita inayomtaka amiri jeshi mkuu aingie kwenye uwanja wa mapambano. Ukikaa na kuagiza nini kifanyike wakati wa mapigano, unajitengenezea kiota cha kushindwa na kuyaona maisha machungu.

 

Sikuachi bila hili; jinsi ulivyo inatokana na namna unavyojitoa katika mapambano ya kimaisha, hatima ya maisha yako ya leo na yajayo, yanategemea sana aina na staili ya kuishi uliyoichagua, ndiyo kusema kufanikiwa au kushindwa katika jambo lolote, mchawi huwa mhusika na hakuna haja ya kutupa lawama kwa wengine.

 

Nilishaeleza huko nyuma. Kila unayekutana naye njiani, anawaza maisha mazuri na ubora timilifu ili afurahie na kufaidi kuzaliwa kwake. Malengo na matarajio huwa makubwa na hakuna awazae kuishi maisha ya hovyo.
Wapo watu wenye ndoto, malengo na maono makubwa mno vichwani mwao. Wanatamani kufikia vilele mbalimbali vya kimafanikio maishani. Kimsingi ukiwasikiliza kwa makini, utagundua kabisa wanayo nia thabiti na wamedhamiria kupigania ndoto wanazoziota usiku na mchana.

 

Hata uwezo wao katika kutenda mambo, ni mkubwa jambo ambalo huondoa shaka juu ya ufanikishaji wa malengo hayo. Unakuta mtu ana akili na uwezo mkubwa mno. Kama ni kwenye masuala ya sheria ni mbobezi, uwezo wake wa kuchambua na kueleza vifungu vya sheria ni mkubwa na hata ‘nondo’ alizonazo kichwani juu ya sheria ni toshelezi kutimiza malengo na ndoto za kuwa jaji mkuu, kwa mfano.

 

Vivyohivyo kwenye maeneo mengine. Tatizo kubwa ambalo huwakwamisha wengi kushindwa kutimiza malengo na ndoto zao maishani ni tabia. Zipo tabia ambazo bila kuondoka maishani kamwe mtu hawezi kufanya chochote au kufika mahali popote. Pia zipo tabia ambazo mtu asipoziingiza maishani mwake, hakuna kinachoweza kufanyika, zaidi ya kuishia kuonesha uwezo mkubwa na kuwafaidisha wengine ambao hawana neema ya uelewa na utambuzi wa mambo, kama
alivyo mhusika. Tukianza na eneo la kwanza la kuondoa tabia fulani ili mtu atimize anachokitaka, tuingie katika uchambuzi yakinifu na wenye kueleweka kwa mapana na marefu manyoofu. Zipo tabia ni lazima uachane nazo ili uweze kufika uendeko. Ni kama ilivyo kwa wapiganaji wa masumbwi, kwamba ili waendelee kuwa na afya stahiki na uwezo mkubwa, ni lazima waachane na aina fulani ya vyakula.

 

Mtu mwingine akila hakuna tatizo kabisa, lakini kwa bondia vitakuwa na madhara na wakati mwingine kushusha na kupunguza uwezo wake ulingoni. Hata katika maisha iko hivyo. Zipo tabia ambazo utake usitake ni lazima uachane nazo, kama kweli umedhamiria kufika mbali katika mbio zako za kusaka mafanikio.

 

Kama wewe ndoto zako ni kuwa mwandishi wa habari, hakikisha unaachana na tabia za uropokaji hivyo na badala yake uwe msikilizaji na mtu wa kujifunza zaidi. Tabia kama ulevi wa pombe na madawa mengine, kamwe haviwezi kuwa rafiki katika mazingira ya mtu kufika mbali kimaisha. Yupo daktari bingwa na maarufu sana duniani, anaitwa Ben Carson. Akiwa kijana mdogo kabisa, alikuwa akishika nafasi ya mwisho darasani kwao na
kila mtu kuanzia wanafunzi wenzake hadi walimu walimuita mjinga.

 

Lakini pia, ujinga wake darasani ulichangiwa na tabia yake ya kutopenda kusoma na badala yake alikuwa mtu aliyependa sana kutazama luninga na kutumia muda mwingi katika michezo ambayo haikuwa na tija maisha mwake. Pia hakuwa mtu wa kusoma vitabu wala kujikumbusha yale yaliyofundishwa darasani.

 

Tabia hizo zilikuwa chachu ya Ben kuonekana mjinga darasani, ingawa katika uhalisia alikuwa na uwezo mkubwa mno, kushinda wanafunzi wote darasani. Kufupisha stori, ni kwamba Ben alipoamua kuachana na tabia hizo kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa mama yake, hatimaye aliingiza tabia ambazo ziliendana na uwezo wake ikiwemo kusoma vitabu na kujifunza mambo mbalimbali, hadi kufikia hatua ya kuwa mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa darasani mwao na shule nzima. Kupitia kwa Ben utakuwa umejifunza kitu. Kitu chenyewe ni kubadilika, kuachana na tabia zote ambazo zimewakwamisha wengi kufikia malengo yao. Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

Makala na Amran Kaima

Comments are closed.