TADB, BoT Zazindua Programu ya Mafunzo Kuboresha Ukopeshaji Sekta ya Kilimo
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Chuo cha Benki Kuu (BoT Academy) wamezindua programu ya mafunzo udhibiti wa wataalamu katika ukopeshaji sekta ya kilimo.
Lengo la programu hiyo ya mafunzo, ni kuchochea upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia ukopeshaji wenye tija. Programu hiyo inatarajia pia kuongeza upatikanaji wa wataalamu wa ukopeshaji katika sekta ya kilimo. Wataalamu hao wanahitajika kwa ajili ya kusaidia kuleta muunganiko wenye tija kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, wakopeshaji na wadau wengine katika sekta.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo katika ofisi ndogo ya BoT jiji, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Frank Nyabundege alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza wataalamu wabunifu, wavumbuzi na wenye uelewa mpana katika suala la ukopeshaji kwenye sekta ya kilimo.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa mafunzo yataongeza wataalamu kwenye taasisi za kifedha katika sekta ya kilimo, kubuni bidhaa na huduma rafiki kwa wakulima kwa kuzingatia vihatarishi vilivyopo kwenye ukopeshaji kwenye sekta hiyo. Kwa kufanya hivi itasaidia pia kuleta uwekezaji zaidi kwa wakulima wadogo na wa kati.
“Programu hii ni hatua muhimu katika kuongeza utaalamu wa kiufundi na ubunifu kwa benki washirika wetu na taasisi nyingine za kifedha katika kukopesha sekta ya kilimo. Mchango muhimu wa mafunzo haya ni kusaidia kuongeza uelewa wa utofauti wa mahitaji na mazingira ya ukopeshaji kwenye sekta ya kilimo,” alisema
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Bi. Sauda Kassim Msemo Naibu Gavana Uthibiti na Ustawi wa sekta ya Fedha alisema benki na taasisi za fedha ni wadau muhimu wa mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo unaoendeshwa na TADB na kuongeza kuwa wanatoa mchango mkubwa katika kutoa huduma za kifedha zinazochangia ukuaji wa sekta ya kilimo.
“Hata hivyo, ukosefu wa utaalamu kwenye kubuni huduma, utoaji wa mikopo na kuvielewa viashiria hatari kwenye kufadhili miradi ya kilimo, vinaweza kuendelea kuwa kikwazo katika kutoa mikopo kwa miradi ya kilimo. Kujengewa uwezo kwa wataalamu wa fedha ili waweze kuwa na uwelewa mpana wa kilimo umeonekana kuwa ni jambo muhimu sana,” alisema Naibu Gavana huyo.
Alisema katika kufanyia kazi suala hilo, BoT Academy kwa kushirikiana na TADB wamebuni program hiyo ya mafunzo kwa ajili ya mabenki ya taasisi za fedha zinazokopesha miradi ya kilimo. “Hii itawawezesha kuwasaidia wakulima wadogo, vyama vya ushirika pamoja na wadau wengine wanaofanya kazi katika myororo mzima wa thamani wa kilimo,” aliongeza
Wawezeshaji katika mafunzo hayo watakuwa wakitoka BoT academy wakishirikiana na wataalamu kwengine utoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA). Wataalamu hawa ndiyo ambao pia wameshiriki kuandaa mtaala wa mafunzo.