The House of Favourite Newspapers

TADB Na Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi Watoa Bilioni 1.2 Kusaidia Mradi Wa Uvuvi Tanga

0
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akiwakabidhi wanufaika wa mradi wa uvuvi mkoa wa Tanga mfano wa funguo za boti. Kupitia mradi huo wizara kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa boti 14 za kisasa pamoja na vifaa vya uvuvi vyote pamoja vikiwa na thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa wavuvi wa mkoa wa Tanga kwa mkopo usio na riba.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo imekabidhi jumla ya boti 14 za kisasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa wavuvi mkoani Tanga.

Mkurugenzi wa Fedha wa TADB, Dkt. Kaanael Nnko, alisema boti hizo za kisasa ni sehemu ya mradi mkubwa wa kimkakati unaoendeshwa kitaifa, ukilenga Vyama Vya Ushirika Vya Wavuvi (FICOs), vikundi vya kijamii vya vijana na wanawake (CBOs), watu binafsi na makampuni yanayojihusisha na shughuli za uvuvi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi boti hizo mkoani Tanga, Waziri wa Mifugona Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema kwa ushirikiano kati ya TADB na Wizarani muhimu kuongeza upatikanaji wa mikopo inayokuza miradi endelevu ya uvuvi.

Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Dkt. Kaanael Nnko, akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi boti 14 za uvuvi za kisasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa wavuvi wa mkoa wa Tanga. Boti hizi zimetolewa kwa mkopo usio na riba kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TADB.

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu, jumla ya boti za kisasa mia moja na sitini (160) zenye thamani yaTZS 11.091 bilioni zitatolewa nchi nzima. Boti hizi zina ukubwa tofautitofauti kuanzia mita tano hadi kumi na nne,” Dr.Nnko alisema.

Kupitia mradi huo, Wizara imetoa jumla ya shilingi bilioni TZS  25.175 billioni kwa TADB,  fedha zitakazotumika kuwakopesha wavuvi bila riba.

Vifaa vitakavyotolewa ni pamoja na boti za uvuvi za kisasa / fibre boats, boti kwa wakulima wa mwani na vifaa vitavyowezesha ufugaji wa samaki kwenye vizimba.

“Namshukuru Mhe. Rais  Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye juhudi zake za kuboresha uchumi wa nchi zimeendelea kuzaa matunda . Ni kupitia serikali hii ambapo kwa mara ya kwanza katika sekta ya uvuvi, inapatikana mikopo isiyokuwa na riba, yaani asilimia 0% halisi bila riba. Hii haijawahi kutokea kabisa,”  alisema Waziri Ulega.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega a(wa pili kulia) akimkabidhi Mwantumu Msuka ambaye ni mmoja ya wanufaika wa mradi wa uvuvi mkoa wa Tanga nyavu ya kuvulia. Kupitia mradi huo wizara kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa boti 14 za kisasa pamoja na vifaa vya uvuvi vyote pamoja vikiwa na thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa wavuvi wa mkoa wa Tanga kwa mkopo usio na riba. Kati kati anayeshuhuduhia ni mkuu wa mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba.

Ulega aliushukuru uongozi wa TADB kwa kuendelea kusaidia sekta ya uvuvi hapa nchini na kuongeza kuwa ushirikiano huo wa kimkakati na TADB utachagiza kukuza sekta ya uvuvi na kuwezesha wadau wake kukuza miradi endelevu na yenye tija zaidi.

Waziri Ulega alibainisha kuwa mikopo hiyo inayotolewa ni uthibitisho wa nia ya dhati ya serikali kuleta mageuzi chanya ya uvuvi nchini.

“Serikali itaendelea kufanyakazi na wadau wote muhimu katika kutekeleza majukumu yake, kuhakikisha upatikanaji wa nyenzo,  rasilimali,  fedha na utaalam utakaochangia mageuzi ya sekta ndogo za ufugaji na uvuvi nchini,” alisema.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega(kati kati) akimsikiliza Mkurugenzi msaidizi wa Huduma za ughani wa uvuvi kutoka wizarani Anthony Dadu (kulia) wakati akilelezea matumizi ya baadhi ya vifaa vya uvuvi wa kisasa muda mfupi bada ya Waziri kukabidhi boti 14 za kisasa kwa wavuvi wa mkoa wa Tanga zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Tanga Waziri Kindamba.

Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa boti hizo, Khamisi Suleiman alisema boti hizo za kisasa zitawezesha kwenda kwenye maji marefu na hivyo kuongeza kiasi cha samaki wanachovua na pia ufanisi.

“Napenda kuwahakikishia kuwa sasa tunaenda kutekeleza shughuli zetu kwa ufanisi mkubwa, tukitambua umuhimu wa kujituma zaidi kazini na kurejesha mikopo kwa wakati ili wengine nao wanufaike,” alieleza

Baadhi ya boti za kisasa za uvuvi zilizotolewa kwa wavuvi wa mkoa wa Tanga kwa mkopo usiokuwa na riba kwa ushirikiano kati ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

TADB inawakaribisha wote wanaojishughulisha na uvuvi, wakulima wa mwani,  wajasiriamali wadogo, vyama vya ushirika, mashirika ya kijamii na wadau wengine wote wa sekta hii sasa kuchangamkia fursa hii ya kipekee ya mikopo isiyokuwa na riba inayopatikana nchi nzima.

Leave A Reply