The House of Favourite Newspapers

TAHADHARI YA KUCHUKUA KWA HOMA YA INI!

UGONJWA wa homa ya ini huambukizwa kwa njia ya virusi ambavyo vikishaingia mwilini, hushambulia ini na usipodhibitiwa mapema hugeuka kuwa ugonjwa sugu. 

 

Virusi vya ini viko katika makundi mbalimbali ambayo ni Hepatitis A, Hepatitis B, Hepatitis C na Hepatitis D. Virusi hivi vinapoingia ndani ya mwili huchukua siku 45 mpaka siku 90 kukomaa, ndani ya siku 60 mtu anapopimwa homa ya ini tayari huwa inajionyesha kuwepo ndani ya mwili.

 

Virusi hivi vinapozaliana kwa wingi ndani ya ini hubadilisha mfumo wa kawaida wa ufanyaji kazi wa ini na kumfanya mtu apate kansa ya ini ambayo husababisha kifo kwa watu wengi.

Ili wananchi waweze kujinusuru na ugonjwa huu kuna haja ya elimu kuendelea kutolewa na watoa huduma ya afya kila mara ili kujenga uelewa wa namna ya kujikinga. Ugonjwa huo unazo dalili zake lakini pia una tiba na madaktari na wataalamu wengine wa afya wana nafasi ya kutoa ushauri kwa wananchi juu ya ugonjwa huo ambao virusi vyake kitaalamu huitwa Hepatitis B Virus (HBV).

 

Virusi vya homa ya ini husambazwa kwa njia ya damu, mwingiliano wowote wa damu kutoka kwa mtu mwenye virusi kwenda kwa mtu mwingine, pia majimaji mengine ya mwilini mfano mate na jasho huweza kupitia huko au huambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa. Kwa maana nyingine ugonjwa huu ukitazamwa kwa kina maambukizi yake yanawiana na ya virusi vya Ukimwi.

 

Hakuna asiyefahamu kuwa virusi vya Ukimwi huambukizwa kwa njia ya kushirikiana vifaa vyenye ncha kali kama wembe, sindano na kujamiiana na mtu mwenye maambukizi bila kutumia kinga. Ugonjwa wa homa ya ini umekuwa hatari kwa sababu una virusi vyenye uwezo wa kuishi nje ya mwili wa binadamu, wakati virusi vya Ukimwi haviwezi kuishi nje ya mwili wa binadamu hata kwa dakika moja.

 

Hivyo ueneaji wa virusi vya homa ya ini ni rahisi zaidi kuliko vile vya Ukimwi. Sasa ugonjwa huu usipodhibitiwa ni hatari kwa afya za watu. Imefika wakati kwa wananchi kulitafakari hili na kuanza kuchukua hatua ya kupima afya zao kila mara.

Ama wanapoona kuna dalili ya homa kali, kupungua uzito au kukosa hamu ya kula, mtu kupatwa na maumivu makali ya tumbo upande wa ini wawahi hospitali. Dalili nyingine ni mtu kujisikia mchovu wakati wote, kupata kichefuchefu, macho, ngozi na viganja vya mikono vinakuwa vya njano na kutapika damu.

 

Virusi vya Hepatitis B huongezeka na kushambulia ini kiasi cha kusababisha uharibifu kabisa kwa ini. Pia ugonjwa huu huweza kusababishwa na fangasi, unywaji wa pombe, dawa, magonjwa yanayosababishwa na kinga ya mwili kuushambulia mwili na magonjwa ya kimetaboliki.

 

Mtu huweza kuupata kwa kula kinyesi kilichochanganyika na vimelea vya ugonjwa huu kwenye maji au chakula. Hata hivyo suluhisho la tatizo hilo ni kujikinga tu dhidi ya sababu za ugonjwa wa homa ya ini kwa kupata chanjo. Kwa bahati nzuri ugonjwa huu una chanjo na mpaka sasa hospitali mbalimbali ikiwemo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili inatoa. Pia ni muhimu watu kujikinga kwa kuepuka kuchangia vifaa vya ncha kali kama sindano, wembe, miswaki na mavazi.

Comments are closed.