The House of Favourite Newspapers

Taharuki: Polisi Wazingira Makao Makuu ya CUF Zanzibar

 

TAHARUKI imeibuka mjini Zanzibar baada ya jeshi la Polisi visiwani humo kuzingira makao makuu ya ofisi ya Chama cha Wananchi (CUF) kwa madai kuwa wamepewa taarifa kwamba kuna mpango wa uvamizi.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro kupitia ukurasa wake wa Facebook ameandika kuwa ‘polisi wana ajenda mbili; kuishikilia kimabavu ofisi hiyo au kuweka vitu vya hatari na kisha kuwakamata viongozi wa chama hicho’.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali amethibitisha polisi kulizunguka jengo hilo.

“Ni kweli kwamba tumeliweka chini ya ulinzi jengo la ofisi za CUF, kwa sababu  kuna viashiria vya watu kufanya uhalifu katika ofisi ya CUF ya Mtendeni na tumeweka ulinzi kwanza. Pia tuhahitaji kuingia ndani ili kuthibitisha maneno yanayosemwa ili kama ni kweli tujue tunakabiliana vipi,” alisema Kamanda Hassan.

 

Mtatiro yeye alisema, “Polisi wakiwa na magari kadhaa, wameivamia makao makuu ya CUF  Mtendeni, Zanzibar saa 12:10 jioni hii. Inaonekana na inahisiwa wana ajenda mbili. Moja ni kuikalia makao makuu hiyo kimabavu ili kesho Jumatatu waikabidhi kwa bwana yule ili kutekeleza mkakati maalum, au wana lengo la kuingia kimabavu na kuweka vitu hatari na kisha kuwakamata viongozi wa CUF na kudai walitunza vitu hatari ofisini hapo. Tunafuatilia jambo hili kwa ukaribu.”

Comments are closed.