The House of Favourite Newspapers

Taifa Stars Vs Malawi Kinawaka Leo

0

LEO Jumapili, tunatarajia kushuhudia mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopo kwenye Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambapo wenyeji Tanzania maarufu Taifa Stars, wakiwakaribisha Malawi ‘The Flames’.

 

Tayari Malawi wameshatua Dar tangu juzi ijumaa kwa ajili ya mchezo huo ambapo jana jioni walifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar ambao utatumika kwa mechi hiyo.

 

Ni mchezo ambao kila mmoja anahitaji ushindi, licha ya kuwa ni wa kirafiki, lakini ni wa kuongeza viwango kwenye renki za FIFA.

 

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, ameuzungumzia mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu hizo kufahamiana vizuri.

 

“Mchezo huu ni muhimu sana kwetu, kwa kuwa utatupa nafasi ya kuangalia ni wapi tumefikia na ni kipi ambacho wachezaji wetu wamekipokea katika siku hizi nane tulizokuwa kwenye kambi.

“Katika mchezo huu tutaangalia zaidi maendeleo na ubora wa mchezaji mmoja mmoja, hivyo tunatarajia kuwatumia wachezaji wengi kadiri iwezekanavyo.

 

“Malawi ni miongoni mwa timu zilizopo kwenye nafasi nzuri katika viwango vya ubora wa FIFA, na wanatarajia kushiriki michuano ya AFCON, hivyo ni wapinzani sahihi kwetu,” alisema Kim.

 

Naye Nahodha wa Taifa Stars, John Bocco, alisema: “Kwanza tunamshukuru Mungu kwa maandalizi ambayo tumeyafanya mpaka sasa, tunajua hautakuwa mchezo rahisi kwetu kutokana na ubora wa wapinzani wetu, lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaibuka na ushindi kwenye mchezo huu.

 

VIWANGO VYAO

Wenyeji Taifa Stars ikiwa nafasi ya 137 kwenye viwango vya soka duniani, inakwenda kupambana na Malawi iliyopo nafasi ya 115.

MATOKEO

Katika mechi sita za hivi karibuni ambazo timu hizo zimekutana kwenye zile za kirafiki na kimashindano, rekodi zinaonesha kwamba, Taifa Stars imeshinda tatu, sare mbili na kupoteza moja.

 

Mara zote ambazo Taifa Stars imeshinda, ilitoka uwanjani na clean sheet, huku pia Malawi nayo kwenye ushindi wake mmoja, ilitoka na clean sheet.

 

Rekodi nyingine ya wawili hawa kukutana inaonesha kwamba, hakuna mechi iliyozaa mabao zaidi ya mawili, hivyo inadhihirisha wazi kwamba timu zao zote ni imara kwenye safu ya ulinzi.

Leave A Reply