Taifa Stars Yaanza Kujifua Misri, Makocha Wapya Wajiunga – Video
TAYARI kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambacho kitaivaa Uganda katika mechi ya kuwania kucheza AFCON siku chache zijazo, kimeanza maandalizi.
Chini ya Kocha Msaidizi, Hemed Morocco, Taifa Stars imeanza mazoezi ya gym na uwanjani huku kocha mpya wa viungo na wataalamu wa masuala ya video wakiwa wamejiunga na kuanza kazi na kikosi hicho.
Kundi la kwanza lilitua mjini hapa juzi likiwa na wachezaji wa ndani wakiongozwa na Aishi Manula na wanaocheza nje wakiongozwa na Saimon Msuva.
Mji wa Ismailia uko Mashariki mwa Misri katika ukanda wa Mfereji wa Suez na hali ya hewa ni baridi. Uganda wamechagua kutumia uwanja wa hapa kutokana na viwanja vyao kutokuwa na vigezo vya CAF.
Nahodha Mbwana Samatta, alitarajiwa kuwasili jana mchana huku wachezaji wa Yanga waliokuwa na jukumu la kimataifa juzi wakitarajia kuwasili leo wakiwa wameongozana na Feisal Salum.
Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche naye anatarajia kuongozana na wachezaji hao na kuja kuanza kazi moja kwa mjini hapa.
Hoteli waliyofikia iko katika eneo lenye ulinzi mzuri kwa kuwa ni mali ya Jeshi la Misri na ni kubwa zaidi mjini hapa.
Mazingira ya kambi kwa kifupi ni yaliyokamilika kwa kuwa hoteli hii inamiliki viwanja bora viwili vya kisasa kwa ajili ya mazoezi, gym kubwa mbili za michezo lakini maeneo makubwa maalum kwa ajili ya kukimbilia kama timu itataka kufanya mazoezi ya nje.
MWANDISHI WETU, ISMAILIA, GPL