The House of Favourite Newspapers

Tajiri aliyeua dereva wake kwa risasi atoroshewa Canada

0

IMG_0674Marehemu David Kalungula enzi za uhai wake.

Stori: Waandishi Wetu, UWAZI

DAR ES SALAAM: Bosi mwenye asili ya Kihindi wa Kampuni ya Triple A Haulers Ltd, inayosafirisha mafuta ya petroli mikoani na nje ya nchi, Hussein Jeta (29) aliyekamatwa na polisi kwa tuhuma ya kumuua kwa kumpiga risasi dereva wake, David Kalungula 36, (pichani), Oktoba 19, mwaka jana, Mbagala Mission, Dar anadaiwa kuachiwa huru na kuna tuhuma kwamba ametorokea nchini Canada.

Taarifa hiyo imewashitua wananchi wengi ambao walisema kuwa, kitendo hicho ni jipu linalosubiri kutumbuliwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’.
Taarifa kutoka chanzo chetu makini ndani ya Jeshi la Polisi Kituo cha Chang’ombe, Temeke, Dar ambacho kilikuwa kikishughulikia sakata hilo zinadai, Jeta aliachiwa Desemba 7, mwaka jana ikiwa ni siku 42 tangu akamatwe.

Chanzo hicho kililieleza gazeti hili kwamba, siku ya tukio, Jeta alikamatwa na watuhimiwa wengine saba, lakini hata hivyo, watano waliachiwa na Polisi wa Kituo cha Chang’ombe na kabaki Jeta na Ali Bimji (26).
Watuhumiwa hao kesi yao ya kudaiwa kuua ilifikishwa Mahakama ya Wilaya Temeke na kupewa Namba ya Kumbukumbu P17/2015 ambapo walipelekwa Mahabusu Gereza la Keko, Novemba 2, mwaka jana.

kitwangaWaziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh Charles Kitwanga.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, Desemba 7, mwaka jana, Jeta aliachiwa huru, akabaki Ali kama mtuhumiwa wa mauaji jambo ambalo baadhi ya polisi wa Chang’ombe wanadai kesi hiyo imefanyiwa ‘ufundi’.

Pia polisi hao walidai kuwa, upelelezi wao ulimtia hatiani Ali kama mmiliki wa bastola kwani inadaiwa alinyang’anywa na Jeta na akaitumia kumfyatulia risasi mbili David.

Chanzo kilisema kesi za mauaji haziendi haraka hivyo ambapo ndani ya mwezi mmoja mtuhumiwa amechomolewa kabla ya upelelezi kukamilika. Pia mahakama ya wilaya haina uwezo wa kusikiliza kesi ya mauaji zaidi ya mahakama kuu lakini barua ya kumtoa mahabusu Jeta inadaiwa kuandikwa na afisa mmoja wa Polisi Temeke na kugongwa muhuri na Mahakama ya Wilaya Temeke.

“Tunamuomba Rais Magufuli na Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kufuatilia sakata hili kwani kuna tatizo la wazi kabisa na wananchi wamekuwa wakihoji kulikoni wakati ilitangazwa bosi huyo alikamatwa,” alisema dereva mmoja wa kampuni hiyo akiomba hifadhi ya jina lake.

Uwazi lilimtafuta kwa njia ya simu, Mkuu wa Gereza la Keko, ACP Mbwana Sinashida ambapo alipoulizwa kuhusu kuachiwa kwa mtuhumiwa Jeta alikiri kuondolewa katika kesi hiyo na kubaki Ali.
“Nilipokea barua kutoka Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwamba, nimuachie Hussein Jeta. Desemba 7, mwaka jana nilimuachia kwa taratibu na sheria kama ilivyoandikwa kwenye barua hiyo. Kesi hii imebaki kwa Ali na itatajwa Mahakama Kuu Jumanne ijayo (leo), ”alisema mkuu huyo wa gereza.

Uwazi ilipiga hodi kwenye ofisi za kampuni hiyo, Mbagala na kukutana na Meneja Uajiri, Solomon Mahogo. Alipoulizwa alipo Jeta, alisema hajafika ofisini hapo tangu akamatwe kwa tuhuma za mauaji na hajui alipo ila wenzake aliokamatwa nao, waliachiwa na wanaendelea na kazi.

maguRais Magufuli.

“Walikamatwa wengi, wakachujwa na Polisi Chang’ombe, wakabaki Jeta na Ali ambao walifikishwa mahakamani lakini hawakupewa dhamana kutokana na kesi yenyewe hivyo walipelekwa Mahabusu ya Gereza la Keko, sijui kinachoendelea,” alisema meneja huyo.

Nje ya ofisi hizo kulikuwa na malori ambayo yalikuwa yakikwanguliwa nembo na hakukuwa na mfanyakazi aliyekuwa tayari kueleza sababu ya kufanya hivyo.

Jumamosi iliyopita, Uwazi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Gilles Muroto na kumuuliza juu ya kuachiwa kwa Jeta ambapo alisema hana taarifa ya kinachoendelea juu ya kesi hiyo.
“Mimi ni mgeni hapa Temeke, nina siku mbili tangu nihamie, sina ninalolijua, ila nitafuatilia,” alisema Kamanda Muroto.

ACP Muroto amehamishiwa Temeke hivi karibuni kuchukuwa nafasi ya ACP Andrew Satta ambaye amehamishiwa Polisi Kanda Maalum ya Tarime-Rorya mkoani Mara.

Marehemu David anadaiwa kupigwa risasi katika ofisi za kampuni hiyo muda mfupi baada ya kutoka safari ambapo ilidaiwa kuwa, alikutwa na upotevu wa lita 70 za mafuta ndipo kukawa na malumbano na bosi wake huyo.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa nyumbani kwao, Mbeya kwa mazishi na ameacha mke na watoto watatu.

Habari hii inaendelea kufuatiliwa kwa undani kama alivyosema Kamanda Muroto na majibu yatapatikana wakati wowote.

Leave A Reply