TAJIRI BONGO ALIYEUAWA KIKATILI NA AL-SHABAAB MALI ZAKE ZASHTUA

MAHAD Abdillah Nur, mfanya-biashara tajiri na mwekezaji Bongo hakuwa amejulikani na wengi hadi pale taarifa za kifo chake ziliposambaa na kuanikwa sehemu ya maisha yake na mali alizokuwa akimiliki.  Tajiri huyo kijana (48) aliuawa Julai 12, mwaka huu katika Jiji la Kismayo nchini Somalia katika shambulio la bomu linalotajwa kufanywa na kundi la Al-Shabaab. Katika shambulio hilo watu wengine 26 wakiwemo Watanzania wawili wanadaiwa kuuawa baada ya kutokea mlipuko mkubwa kwenye hoteli ya Asasey.

MALI ZA MAHAD ZASHTUA

Baada ya mauaji hayo kutokea watu mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete waliandika masikitiko yao kwenye mitandao yao ya kijamii kuhusiana na kifo cha Mahad.

Aidha, baadhi ya watu waliodai kumfahamu mfanyabiashara huyo walisema alikuwa mtu muhimu kwa taifa huku wakiainisha baadhi ya mali walizodai kuwa marehemu alikuwa mmoja wa wamiliki wake. Mali hizo ni pamoja na Paradise Holiday Resort ya Bagamoyo (iliyoungua miaka kadhaa iliyopita), Mgahawa wa City Garden, Italy Shoe,Tansoma Hoteli, City Mall na Victoria Plaza zote zikiwa sehemu mbalimbali katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam.

Ingine ni Maisha Supermarket ambayo marehemu Mahad alikuwa mkurugenzi mtendaji wake hadi umauti unamfika. Taarifa hii ni kwa mujibu wa meneja wa supermarket hiyo, Emodia Lloyd alipozungumza na UWAZI.

Kutajwa kwa sehemu ya utajiri huu wa Mahad kuliwashtua watu wengi ambapo hapo awali walikuwa hawafahamu kuwa kijana huyo aliyeingia nchini miaka ya 90 akitokea Somalia kukimbia machafuko alikuwa na utajiri huo mkubwa.

IDADI YA WATANZANIA ALIOWAAJIRI

Ingawa idadi kamili ya Watanzania aliowaajiri mfanyabiasha huyo haikutajwa; lakini kupitia uwekezaji wa majengo na biashara mbalimbali alizokuwa akizifanya ni wazi kuwa alikuwa ametoa ajira kwa Wabongo wengi.

“Ni pigo sana kwa uchumi wa nchi yetu kwani alikuwa ni mwekezaji ambaye alichangia kuzalisha ajira kwa wengi, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” aliandika mmoja wa wamiliki wa ukurasa wa Instagram.

AACHA SIMANZI

Albert Kawogo mmoja kati ya waandishi wa habari mahiri na wakongwe nchini aliandika kwenye ukurasa wa Facebook kuwa: “Tulikaa vema Bagamoyo nakumbuka mwaka 2008 nilikuaga naelekea Khartoum Sudan kwa kazi ya habari ila sina kamera, ulinipa … nikanunua kamera aina ya Sony pale Mlimani City, ulikuwa ni rafiki jirani na mshikaji mwema.”

Naye mmoja kati ya wafanyakazi wa Maisha aliyejitambulisha kwa jina moja la Said alimwambia mwandishi wetu kuwa Mahad alikuwa mtu mwenye upendo aliyewajali na kuwapenda wafanyakazi wote bila ubaguzi.

Kama hilo halitoshi baadhi ya waandishi wa habari ambao mara kadhaa walikuwa wakikutana Bagamoyo kwenye Hoteli ya Paradise walimwelezea Mahad kuwa alikuwa ni kijana asiyekuwa na majivuno. “Tuliwahi kwenda pale kushiriki mkutano ulioandaliwa na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), usiku yule kijana hakulala alikuwa anatuzungukia kwenye meza na kuongea nasi kwa upendo, ilikuwa vigumu kuamini kama ndiye aliyekuwa mmiliki wa hoteli,” alisema Elvan Stambuli mmoja kati ya waandishi wa habari wakongwe nchini.

MAHAD ALIKWENDA SOMALIA KUFANYA NINI?

Taarifa zilizotolewa na Meneja wa Maisha, Emodia alisema kuwa mfanyabishara huyo alikwenda nchini humo kwa shughuli zake za kibiashara. Hata hivyo, hakufafanua zaidi ingawa inaelezwa kuwa aliondoka na rafiki yake mmoja kutoka hapa nchini ambaye naye amedaiwa kuuawa katika shambulio hilo baya kuwahi kufanywa katika jiji hilo la Kismayo.

KWA NINI AL- SHABAAB WASHAMBULIE HOTELI HIYO

Vyanzo mbalimbali kutoka katika mitandao ya kijamii vimedai kuwa huwenda shambulio hilo lilifanywa na Al-Shabaab kwa sababu za kisiasa. Itakumbukwa kuwa tangu machafuko yaliyomwagusha Rais wa Somalia, Jenerali Siad Barre miaka ya 90 hali ya utulivu haijapata kutokea kutokana na kuwepo kwa makundi mengi ya waasi wakiwemo Al-Shabaab wanaowania uthibiti wa mji mkuu wa Mogadishu.

Wachambuzi mbalimbali wa mambo ya kisiasa wamelielezea shambulio hilo kama lilifanywa baada ya Al- Shabaab kuhisi kulikuwa na mipango ya kisiasa iliyokuwa ikifanywa kwenye hoteli hiyo. Inafahamika kuwa miongoni mwa watu waliouwa ni pamoja na maofisa wa serikali ya Somalia akiwemo mgombea urais katika jimbo lililojitenga la Jubaland.

Aidha, baadhi ya watu waliouawa wametajwa kuwa wametoka katika mataifa ya Kenya, Marekani, Uigereza, China na Canada ambayo yamekuwa yakipinga vitedo vya kigaidi vinavyoendeshwa na Al-Shabaa huku kisingizio cha kupigania dini ya Kiislamu kikitumiwa na waasi hao mara kadhaa.

Kutokana na mtazamo huo huwenda raia wa nchi hizo na baadhi ya viongozi wa serikali ya Somalia walikutana kwenye hoteli hiyo katika mipango ya kisiasa. Hata hivyo, haikufahamika kama Mahad alikuwa miongoni mwa watu hao wanaohisiwa kukutana kisiasa au alikumbwa na mtego wa Al-Shabaab usiomhusu.

MAHAD NI NANI?

Ni raia wa Somalia ambaye alikimbia machafuko nchini mwake miaka hiyo ya 1990 na kuja kuishi eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam. Anatajwa kuchanua kibiashara yeye, washirika na familia yake baada ya kuanza kufanya uwekezaji na kuendesha miradi mbalimbali tangu enzi za uongozi wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Kutokana na fursa hiyo kijana huyo ambaye sehemu ya familia yake inaishi hapa nchini na nyingine Somalia, amekuwa akiishi hapa na wakati mwingine akirejea nyumbai kwao kwa sababu za kifamilia au za kibiashara.

Hadi kifo kinamfika, alikuwa amefanya uwekezaji mkubwa nchini wa majengo, miradi na biashara huku akitajwa kuwa alikuwa mbioni kuitoa moja kati ya makampuni yake kuidhamini timu ya Simba ya jijini Dar. Taarifa ambazo zimelifikia UWAZI wakati likienda mtamboni bila kuthibitishwa na mamlaka husika kutokana na maofisa habari wa wizara ya Mambo ya Nje kutopatikana ni kwamba mwili wa Mahad ulizikwa nchini Somalia, Julai 13 mwaka huu.


Loading...

Toa comment