The House of Favourite Newspapers
gunners X

Takukuru Siha Kuwafikisha Mahakamani Watendaji Waliokwamisha Miradi Ya Serikali

0
Mkuu wa  Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Siha, Deo Mtui akizungumza na waandishi.

 

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro imeanza uchunguzi wa manunuzi hewa ya vifaa vya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na ubadhirifu wa fedha zaidi ya shilingi Mil 80,000,000/= za serikali zilizosababisha kushindwa kukamilisha ujenzi wa majengo mapya saba ya hospitali hiyo ambayo mpaka sasa hayajaanza kufanya kazi kama ilivyotarajiwa.

 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa  Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Siha, Deo Mtui alisema taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi kwa awamu ya pili katika hospitali hiyo ambapo katika awamu ya kwanza walibaini ubadhirifu kwa mzabuni ambaye alinunua vitasa duni vya milango hivyo kuamriwa na taasisi hiyo kurudisha fedha zaidi ya shilingi Mil 11,000,000/= ili iweze kununua vitasa vyenye ubora ambapo alifanikiwa kurejesha fedha hizo.

 

“Awamu hii kazi ambayo tunaendelea nayo ni kwamba tuchunguza zaidi ya shilingi milioni 80 ambapo katika fedha hizo  tunachunguza fedha kiasi cha shilingi milioni 16 ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya kulipa mafundi na kiasi cha shilingi milioni 27 ambazo zilitumika kufanya malipo hewa ya vifaa hewa na kiasi cha shilingi milioni thelathini (30)tunazoendelea kuchunguza ni fedha ambazo zimetumika kizembe kununua vifaa vingi ambavyo vilikuwa havihitajiki.”Alisema Mtui

Mkuu wa wilaya ya Siha, Onesmo Buswelo akifafanua jambo.

Mkuu wa wilaya hiyo Onesmo Buswelo akizungumzia sakata hilo alisema kama pamoja na kumshukuru Rais Dkt. John Pombe Mgufuli kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni moja nukta tano kwa ajili ya kujenga majengo mapya ya hospitali ya wilaya walikumbana na changamoto kadhaa ambazo baada ya majengo hayo kutokamilika kwa wakati jambo ambalo walitilia shaka uadilifu na uamifu wa baadhi ya watumishi waliopewa dhamna ya kusimamia ujenzi huo.

 

Alisema walipata mashaka kwenye maeneo ya uagizaji wa vifaa, upokeaji na kwenye malipo jambo ambalo lilisababisha kamati ya usalama kuelekeza (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa kina lakini pia kumuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Ndaki Mhuli kupitia mkaguzi wa ndani kufanya uchunguzi kuona ni wapi fedha hizo zimeishia.

 

“Katika fedha hizo tulitarajia ibaki kiasi cha shilingi milioni mia moja kumi na nane 118,000,000 shs kwa ajilia ya njia za waenda kwamiguu hospitalini hapo lakini cha ajabu ilipofika januari mwaka huu mkurugenzi alisema hana fedha na kazi haijaisha hivyo uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kulikuwa na udanganyifu kwa mhandisi pamoja na timu yake.”Alisema Buswelo.

 

Alisema katika uchunguzi wa awali ilionesha kuwa mhandisi na timu yake walifanya udanganyifu wa fedha zote walizotakiwa kulipa mafundi na katika kuwalipa zililibaki zaidi ya shilingi Mili 16,000,000/= ambazo hazijulikani zilipo huku zikionesha zipo ofisi ya mhasibu ambako napo hazipo.

 

“Sasa mapungufu hayo pamoja na mengine na ubadhirifu huu tumewapa kazi TAKUKURU na mimi mwenyewe kwa mkono wangu niliwaandikia barua kuwataka kufanya uchunguzi mapema itakavyowezekana na kisha hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika kwa kuwa tunataka fedha za umma zifanye kazi kama ilivyokusudiwa ili itupatie matokeo chanya kama ambayo Mhe Rais na watanzania wanavyotazamia.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmasahuri ya Siha, Ndaki Stephano Mhuli alisema kama halmashauri kwa nafasi yao wamechukua hatua kwa wahusika wote na wameunda kamati ya uchunguzi kwa maana ya taratibu za kinidhamu ili kubaini makosa ya wahusika.

 

Hata hivyo kwa mujibu wa maagizo ya Serikali hospitali zote 67 za wilaya ambazo zilipewa fedha na serikali kiasi cha shilingi bilioni 1.5 zilipaswa kuwa zimekamilika na kuanza kazi ifikapo Machi Mosi 2020, agizo ambalo kwa wilaya ya Siha limeshindwa kutekelezwa kutokana na ubadhirifu huo.

Leave A Reply