Takwimu za Mayele Hatari Sana

UKIWEKA kando kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes kuonja joto ya jiwe kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii, wachezaji walifunika kwenye asilimia kubwa za takwimu huku Fiston Mayele akifunika.

 

Ndani ya dakika 90, wachezaji wa Simba waliweza kupelekeshana mpelampela na vijana wa Nasreddine Nabi wa Yanga katika takwimu huku wakishindwa kutumia vizuri nafasi ambazo walizipata katika mchezo huo.

 

Kwa upande wa safu ya ushambuliaji, jumla Simba ya Chris Mugalu ilipiga mashuti 15 na ni mashuti matatu yalilenga lango huku 12 yakikwama kulenga lango kwenye mchezo huo wa Ngao ya Jamii.

 

Kwa upande wa Yanga yenye Fiston Mayele, ilipiga jumla ya mashuti 11, ni matano yalilenga lango na sita yalikwama kulenga lango na katika hayo matano, ni moja lile la Fiston Mayele lililenga lango na kumshinda mlinda mlango Aishi Manula.

 

Kona, Yanga ilipiga saba hapa iliwapoteza mazima Simba kwa kuwa wao walipiga kona tatu pekee na zote zilipigwa na kiungo wao fundi Rally Bwalya, katika kona hizo mbili zilikuwa na hatari zilipokutana na beki Joash Onyango ambapo ile ya kwanza iligonga nguzo na ile ya pili ilikwenda nje ya lango.

 

Simba ilicheza jumla ya faulo 26 na ni Taddeo Lwanga ambaye alikuwa mkata umeme alikata umeme mpaka akaonyeshwa kadi mbili za njano na kupelekea kuonyeshwa kadi nyekundu huku Yanga wakicheza faulo 18.

 

Kuotea, hapa namba zilikuwa sawa kwa wote Yanga ilikuwa mara moja na Simba ilikuwa ni mara moja pale Uwanja wa Mkapa sawa na ilivyokuwa kwenye kadi za njano ambapo wote walionyeshwa kadi nne za njano.

 

Umiliki wa mpira, Simba iliwapoteza Yanga jumlajumla kwa kuwa walikuwa na umiliki 53, huku wapinzani wao Yanga wakiwa na umiliki asilimia 47, licha ya Simba kuwa na umiliki mzuri wa mchezo ngoma iliisha Simba 0-1 Yanga na Ngao ya Jamii ni mali ya Yanga.

LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam


Toa comment