The House of Favourite Newspapers

Tamasha Kubwa La Injili Kuanza Kesho Dar, Likiongozwa na Muinjilisti Johannes Amritzer

0
Mwinjilisti Johannes Amritzer (wa pili kulia) akizungumza na wanahabari leo kwenye mkutano uliofanyika Viwanja vya Mwembe Yanga Jijini Dar litakapofanyika tamasha hilo.

Muinjilisti wa kimataifa kupitia SOS ADVENTURE, Johannes Amritzer kesho anatarajia kufanya mkutano mkubwa wa Injili ambao utawakutanisha maelfu ya waumini wa dini mbalimbali katika mkoa wa Dar Es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar Es Salaam leo Julai 8, 2024 Muinjilisti Johannes amesema Tamasha hilo linalojulikana kama FURAHA FESTIVAL utafanyika katika Uwanja wa Mwembe Yanga uliopo Temeke Jijini Dar kuanzia kesho Jumanne Julai 9 na utahitimishwa Jumamosi Julai 13, 2024 kuanzia saa 9 Alasiri.

Muimbaji wa nyimbo za injili almaarufu kwa jina la Julia Willkander akimwaga tambo jinsi kesho atakavyofanya vitu vyake jukwaani kwenye tamasha hilo.

Tamasha la Furaha Festival linatarajiwa kuhudhuriwa na watu mbalimbali ambapo litawakutanisha pia wasanii mbalimbali wa muziki wa injili ndani na nje ya nchi akiwemo Boaz Danken, Miriam Mauki Lukindo, Julia Willkander na Rose Muhando ambao watatoa huduma ya uimbaji katika kusanyiko hilo.

Muinjilisti Johannes amesema mkutano huo ni katika shamrashamra za kuelekea katika maadhimisho ya miaka 85 ya Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) ambao ni washirika wenza wa SOS Adventure ambayo yatafanyika uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar Es Salaam Julai 13 mwaka huu siku Moja tu baada ya kumalizika kwa mkutano wa Injili wa Mwembeyanga.

Wanahabari wakiwa kazini kwenye mkutano huo.

“Yesu alituambia Kuna Jambo anataka afanye Dar na akatuuliza Je?mnaweza kwenda nasi?Kwa hiyo kwenye mkutano huu hakuna Star zaidi ya Yesu ambaye atahubiriwa”amesema Muinjilisti huyo na kuongeza,

“Mimi nilikuwa Yatima tangu nikiwa na miaka sita na niliishi mtaani Kwa kipindi kirefu,nilipitia uhuni wote utumiaji wa dawa za kulevya lakini Yesu aliniokoa nilipofikisha miaka 20 hivyo naamini Yesu huyo huyo aliyoniokoa Mimi atafanya Kahaba kuwa Mwanamwali na Chokoraa kuwa bosi,hivyo nawaomba watu wote kufika ili kushuhudia makuu ya Mungu”ameongeza

Aidha Muinjilisti huyo amesema kuwa amekuja na zaidi ya watu 250 pamoja Naye,na tayari wameshatoa misaada katika maeneo mbalimbali ikiwemo taulo za kike (pedi) Kwa wanafunzi wa Shule mbalimbali,kufanya semina Kwa wafanyabiashara na Kula nao chakula Cha jioni ambapo jumla ya Shilingi bilioni 1.2 zimetumika kwenye maandalizi ya mkutano huo ambao unaenda sambamba na kongamano kubwa la vijana linalofanyika katika uwanja wa Uhuru Kila siku kuanzia saa 2 asubuhi.

“Mbali na mkutano huu wa hapa Mwembeyanga Pia tumekuja na vijana kutoka zaidi ya mataifa 15 ya Afrika ambao ni pamoja na wakurugenzi wa mashirika mbalimbali na tunategemea vijana zaidi ya elfu 10 washiriki katika Kongamano la vijana pale uwanja wa Uhuru kuanzia Kesho Julai 9 kuanzia asubuhi ili kuwapa mafunzo na mafundisho mbalimbali “amesema.

Amesema vijana hawawezi kupona na kufanikiwa bila ya kumtanguliza Mungu na Kuitambua Injili ya Yesu Kristo na yeye ndiyo atawapa maisha bora kufungua milango ya mafanikio katika maisha yao Kwa wale waliotayari kumpokea.

Katika Mkutano huo pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ataombewa  kwani mkutano huo humuombea kiongozi yoyote na serikali yake iliyoko madarakani ili Mungu awalinde na walihudumie vyema Taifa.

Kwa upande wao wasanii wa muziki wa Injili akiwemo Miriam Lukindo wa Mauki ambaye ni msaanii nguli wa muziki wa Injili Tanzania na Julia Willkander ambaye ni Raia wa Sweden na kwa sasa anafanya huduma zake nchini Kenya wamewakaribisha watanzania hasa vijana kuhudhuria katika uwanja wa Mwembe Yanga ili kuona Mambo Makuu aliyofanya Mungu na kukombolewa kifikra,kiuchumi na Kijamii.

Furaha Festival itaanza rasmi hapo kesho katika uwanja wa Mwembe Yanga na utahitimishwa siku ya Jumamosi ambapo siku inayofuata (jumapili)Mhubiri Johannes Amritzer atashiriki katika maadhimisho ya miaka 85 ya uinjilishaji wa kanisa la TAG ambayo pia yanatarajiwa kuhushiriwa na Rais Dkt Samia Julai 13,2024 katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Leave A Reply