The House of Favourite Newspapers

Tamasha la Airtel Wasafi Festival 2023 Lawapagaisha Wakazi wa Ruangwa

0
Rais wa WCB na Balozi wa Airtel Diamond Platnumz akifanya vitu vyake katika tamasha la Airtel Wasafi Festival mjini Rungwa, mkoani Lindi jana. Ili kunogesha tamasha aliingia kwa staili ya aina yake akivaa vazi la kizombi.
LIKIWA katika onyesho lake la pili, baada ya Mtwara, Tamasha la Airtel Wasafi Festival linalodhaminiwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel limeendelea kuonesha kuwa ni moto wa kuotea mbali baada ya safari kuutikisa mji wa Ruangwa pamoja na viunga vyake baada ya kushuhudia wasanii wakali zaidi 21 wakilishambulia jukwaa kila mmoja kwa staili ya aina yake.
Wasanii hao wengi wao wakiwa ni kutoka crew ya Wasafi Classic Baby (WCB) walilishambulia jukwaa bila kuchoka wakiongozwa na Rais wa WCB na Balozi wa Airtel Diamond Platnumz ambaye yeye alivunja rekodi kwa kuingiana staili ‘Kizombi’ hivyo kufanya maelfu ya wakazi wa Ruangwa kushingilia kwa nguvu muda wote wakati mkali huyo akishusha ngoma zake zinazobamba katika chati kwa sasa na kupiga shoo ya nguvu akianza kwa kuchagiza akikitaja  jina la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ambaye yeye ni mwenyeji wa Ruangwa na hivyo kuamsha kelele za shangwe kutoka kwa mashabiki wake.
Na kama hiyo haitoshi, mkali mwingine, Rayvvany huyu naye awali akitokea WCB, lakini sasa akimiliki  lebo yake iitwayo ‘Next Level Music’ yeye aliamua kuibadilisha steji kuwa kama yupo kijijini baada ya kuweka jengo la nyumba yenye asili ya kiafrika huku akiwa na mifugo kadhaa, ikiwemo sungura na mbuzi lakini hayo yote ikiwa ni kutia chachandu tamasha la Airtel Wasafi Festival ambalo mwaka huu limekuja kivingine.
Akizungumza, Meneja Mahusiano wa Kampuni ya Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema, kama ilivyoahidiwa siku ya uzinduzi wa tamasha hili, ndicho kinachofanyika kwani Tamasha la Wasafi Festval 2023 chini ya udhamini wa Airtel halifanyiki kwa mtindo wa kimazoea.
“Airtel Wasafi Festival 2023 ni moto wa kuotea mbali, sisi kama Airtel Tanzania tunataka watanzania wapate burudani ya uhakika hususani katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
“Lakini sio burudani tu kutoka crew nzima ya WCB na wasanii wengine bali kila panapofanyika matamasha haya, Airtel tumeendelea kutoa huduma za mtandao wetu bora ikiwa ni pamoja na kufungua maduka ya Airtel Money ili kuweza kusogeza huduma zetu karibu zaidi kwa wateja wetu na kwa watanzania kwa ujumla.
Licha ya burudani ya nguvu kutoka katika steji ya Airtel Wasafi Festival 2023, wahudhuriaji hupata fursa ya kupata huduma mbalimbali kutoka Airtel kama kufanya miamala ya Airtel Money, kusajili laini kama inavyoonekana pichani.
Airtel tunahamasisha watanzania wote wasikose fursa hii ya kuhudhuria kwa wingi katika matamasha haya yanayoendelea kwani Airtel Wasafi Festival 2023 ni zaidi ya burudani,” alisema Bwana Mmbando.
Mara baada ya onesho la Ruangwa tamasha litakalofuata la Airtel Wasafi Festival linatarajiwa kufanyika katika mji wa Songea mkoani Ruvuma, ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi wa Airtel, Diamond Platnumz atafungua Airtel Money Branch, kuhudumia wateja na kufanya shughuli nyingine za kijamii mkoani humo.
Mbali ya Rais huyo wa WCB, baadhi ya wasanii wengine wanafanya makamuzi katika tamasha la Wasafi Festival la mwaka huu ni, Jux, Rayvan, mbosso, Mr Blue, Darasa, Young Lunya, Lavalava, Zuchu, Chid Benz, Billnas, Mabantu, Linex, J Melody, Kusah, Weusi, Chege & Temba na wengine wengi.
Leave A Reply