The House of Favourite Newspapers

Tamasha la Utamaduni na Utalii Kutimua Vumbi Bariadi

0
Baadhi ya wapiga ngoma na waimbaji kutoka Makundi ya Wagika na Wagulu wakipasha ili kujiandaa na Tamasha la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa.

Hatimaye Tamasha la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa – Lake Zone Cultural and Tourism Festival lililokuwa linasubiriwa kwa hamu sasa linatarajiwa kuanza rasmi kesho Julai 5.

Tamasha hilo la aina yake na la kwanza Bariadi, linaloandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours, linatarajiwa kufunguliwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Dunstan Kitandula katika Viwanja vya CCM Bariadi Mjini.

Akizungumza Mjini Bariadi Mkoani Simiyu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro One Travel and Tours, Christina Jengo alisema maandalizi yote yamekamilika na tayari makundi mbalimbali yalikuwa yameshaanza kuwasili mjini hapo tayari kwa tamasha hilo la siku tatu.

“Msisimko ni mkubwa kama mnavyoona makundi yako tayari kuchuana na kuburudisha katika hali ya kudumisha mila za kisukuma hasa wakati wa mavuno yaani mbina,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema Tamasha hilo mbali na kupambwa na mambo mbalimbali ya kimila, pia litaambatana na maonesho mbalimbali ya masuala ya kijadi na pia biashara mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa Utamaduni wa Mkoa wa Simiyu, Buhimila Shala alisema kutakuwa na makundi zaidi ya 25 katika tamasha hilo kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na nje ya kanda hiyo.

“Mipango yote imekamilika tunasubiri tu siku ya kesho tuanze tamasha letu, hata hivyo msisimko tayari ni mkubwa katika Mji wetu wa Bariadi na Mkoa wa Simiyu kwa Ujumla,” alisema.

Mkrugenzi huyo pia alisema kuwa kutakuwa na mambo mbalimbali ya kusisimua kama kucheza na fisi na nyoka ambayo ni kawaida kwa tamaduni za kisukuma.

Tamasha hilo litafanyika Julai 5, 6 na kilele chake ni tarehe 7.

Wadhamini na wadau wa tamsha hilo ni pamoja na NMB Bank, Bodi ya Utali Tanzania (TTB), People’s Bank of Zanzibar (PBZ), Zanzibar Insurance Corporation (ZIC), Z&M General Traders, Widescope Enterprises Limited, na Carehealth and Hospitality Services.

Leave A Reply