Tambwe, Busungu wamchanganya Pluijm
Amissi Tambwe.
Sweetbert Lukonge
KIKOSI cha Yanga kipo katika maandalizi kabambe ya kujiandaa na mechi yake ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga, lakini washambuliaji wake wawili, Mrundi, Amissi Tambwe na Malimi Busungu wameonekana kumchanganya kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Wachezaji hao wanaonekana makali yao ya kuzifumania nyavu yamepungua ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali wakati michuano ya ligi kuu ilipoanza kutimua vumbi.
Kutokana na hali hiyo, Pluijm ameamua kuwaweka sawa kabla ya mechi hiyo ya Jumamosi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa kuwafua vilivyo.
Katika mazoezi ya jana ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar, Pluijm alitumia zaidi ya saa mbili na robo akiwafundisha wachezaji hao jinsi ya kufunga wakiwa wamebaki na beki mmoja.
Wakati wanaanza kufanya zoezi hilo, lilionekana kuwa gumu kwao lakini jinsi muda ulivyokuwa ukisogea, ndivyo walionekana kuimarika na kufanya vizuri pamoja na washambuliaji wengine wa timu hiyo.
Katika hatua nyingine, Pluijm aliwaweka kitimoto mabeki wa timu hiyo na kuwaelekeza jinsi ya kukaba pindi beki mmoja anapobaki na mshambuliaji mmoja au wawili.
Mabeki waliokumbana na balaa hilo ni Mtogo, Vincent Bossou pamoja na Pato Ngonyani.
Inasemekana kuwa Pluijm alilazimika kufanya hivyo kutokana na kuwa na hofu kubwa ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wake wa kutumainiwa katika mechi hiyo ya Jumamosi ambao ni majeruhi.