The House of Favourite Newspapers

Tambwe, Ngoma warudisha mamilioni Yanga

0

SIMBA YANGA (12)

YANGA imesema kiroho safi inaridhika na utendaji kazi wa mastaika wao Donald Ngoma na Amissi Tambwe na kuona kama wamerudisha fedha za usajili walizolipwa hivi karibuni.

Ngoma na Tambwe kila mmoja amefunga mabao manne hadi sasa na kuiwezesha Yanga kukaa kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tano.

Wachezaji hao ukianzia na Ngoma raia wa Zimbabwe na Tambwe kutoka Burundi, imekuwa desturi kwa mmoja wao kufunga pindi Yanga inapocheza na kuchagiza ushindi wa timu yao.

Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha amekiri wachezaji hao kufanya vizuri na wao kama klabu kuona kama wamerudisha fedha za usajili walizolipwa hivi karibuni.

“Tunajivunia kuwa na wachezaji hawa katika kikosi chetu kwani jitihada zao kila mtu anaziona, tunaweza kusema matunda ya fedha zetu tulizozitoa kwao tumeanza kuyapata,” alisema Tiboroha.

“Yaani hapo ni kama wamerudisha fedha walizolipwa  wakati wa usajili kwa maana wakati mwingine unaweza kumsajili mchezaji na usitarajie kupata kile ulichotarajia.”

Ngoma alisajiliwa kutoka FC Platinum ya Zimbabwe kwa dau la dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 100) na Tambwe alipewa dola 30,000 (zaidi ya Sh milioni 60).

Pia Yanga iliwasajili Thabani Kamusoko kutoka Platinum kwa dau la dola 40,000 sawa na Sh milioni 80 na Malimi Busungu kwa Sh milioni 25.

Ikiwa kileleni, Yanga hadi sasa imefunga mabao 12 na ukiacha manane yaliyofungwa na Ngoma na Tambwe, Busungu amefunga mawili, Simon Msuva na Kamusoko kila mmoja amefunga bao moja. Yanga itashuka tena uwanjani Oktoba 17, mwaka huu kucheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam ipo nafasi ya pili katika ligi hiyo ikiwa na pointi 15 pia.

Leave A Reply