TAMISEMI: Madarasa Hujengwa Kwa Kuzingatia Maoteo Na Sio Kusubiria Matokeo
SERIKALI imesema imekwisha badili utaratibu wa kujenga madarasa kwa wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza na kutoa wito kwa watendaji wote kuzingatia utaratibu wa kujenga kwa kufuata maoteo ya ufaulu yanayowekwa na kila halmashauri.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde bungeni jijini Dodoma Februari 9, 2024 kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI wakati alipokua akijibu maswali ya wabunge ikiwa ni kikao cha tisa cha mkutano wa 14 wa Bunge la 12.
“ Kwa wakati huu Serikali imekwisha badili utaratibu wa kujenga madarasa kwa wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza. Shule hufanya maoteo ya ufaulu kwa mwaka na kuwataka watendaji kuanza ujenzi wa madarasa kwa kuzingatia maoteo ya ufaulu yaliyowekwa. Hivyo utaratibu wa kungojea matokeo ya wanafunzi yatoke ndio waanze ujenzi haupo tena,” Amesema Mhe Silinde.
Aidha Mhe Silinde amesema serikali inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu nchini na hivi karibuni itatangaza ajira za walimu baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais-Utumishi kukamilika na kadri ya upatikanaji wa fedha.
Akijibu swali la Mbunge wa Singida Mjini, Mhe Mussa Sima aliyehoji mkakati wa serikali katika kutoa ajira za kutosha kwa walimu, Mhe Silinde amesema,
“ Kwa mwaka 2022 Serikali iliajiri walimu 9,800 wa Shule za Msingi na Sekondari na kwa mwaka 2023 serikali iliajiri walimu 13,130 wa shule za msingi na sekondari.
Serikali inatambua mahitaji ya walimu kote nchini. Hata hivyo kila mwaka inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu katika sekta ya elimu na hivi karibuni baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais-Utumishi kukamilika na kadri ya upatikanaji fedha ajira mpya za walimu zitatangazwa,” Amesema Mhe Silinde.