The House of Favourite Newspapers

Serikali Yatoa Tamko Kuhusu Mpango Wa Uendelezaji Wa Eneo Maalum La Kiuchumi La Bagamoyo

Serikali ya Tanzania imekanusha taarifa zinazozagaa mtandaoni zikidai kwamba kampuni moja kutoka Saudi Arabia imepatiwa mkataba wa ujenzi na uendeshaji wa Bandari ya Bagamoyo.

Kupitia taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, serikali imesisitiza kuwa madai hayo si ya kweli na haijaingia makubaliano yoyote na mwekezaji yeyote hadi sasa.

Waziri Mkumbo ameeleza kuwa, pamoja na uwepo wa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walioonesha nia ya kuwekeza katika mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone (BSEZ), mazungumzo bado yanaendelea na hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa.

BSEZ ni sehemu ya miradi 17 ya kimkakati inayotekelezwa chini ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.

Mradi huu wa kimkakati unajumuisha ujenzi wa bandari ya kisasa, kongani za viwanda, kongani za TEHAMA, ukanda huru wa biashara na kituo cha reli. Serikali inashirikiana na sekta binafsi kupitia mpango wa ubia wa PPP (Public-Private Partnership) ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

“Serikali inashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi na uwazi,” ameongeza Waziri Mkumbo.

Serikali imesisitiza kwamba kwa kuzingatia umuhimu wa mradi wa BSEZ, umma utaendelea kupatiwa taarifa rasmi kwa kila hatua muhimu ya maendeleo yake. Wananchi wametakiwa kupuuza taarifa zisizo rasmi na kufuatilia vyanzo sahihi vya habari.