The House of Favourite Newspapers

Tanasha kuwakutanisha Diamond, Harmonize!

0

 

Mwanamuziki anayekuja resi kwenye muziki wa Kizazi Kipya; Tanasha Donna Oketch, anadaiwa kupanga kuwakutanisha mastaa kibao wa muziki huo wakiwemo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’, Risasi Jumamosi limeinyaka.  Vyanzo vya uhakika vimelieleza gazeti hili kuwa, Tanasha amepanga kufanya tukio hilo atakapokuwa akizindua EP (Extended Play; nyimbo kadhaa kabla ya albam) yake.

Tanasha ambaye ni mzazi mwenza wa Diamond au Mondi, anatarajia kufanya uzinduzi huo Januari 31, mwaka huu jijini Nairobi, Kenya. Wiki iliyopita mwanamama huyo aliachia wimbo wake mwingine mkali wenye jina la La Vie akiwa na msanii wa Bongo Fleva; Mbwana Kilungi ‘Mbosso’.

Katika wimbo huo unaotrendi kwa sasa kwenye YouTube, Tanasha na Mbosso wametumia lugha tatu za Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa katika kufikisha ujumbe wa kimapenzi unaopatikana ndani yake. Wimbo huo umepokelewa vizuri na mashabiki wake Afrika Mashariki kufuatia promo uliopata kutoka kwa mastaa walio chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Mondi ambapo kila mmoja ameuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Akizungumza na gazeti hili juu ya uzinduzi huo, Tanasha au mama Naseeb JR alisema wimbo huo ni kati ya nne zitakazopatikana ndani ya EP yake hiyo. “Ni projekti kubwa, hivyo inahitaji uzinduzi mkubwa. Utafanyika Nairobi na kama mambo yataenda sawa, utafanyika pia Tanzania.

Kuhusu kuhudhuriwa na mastaa wote wakubwa Afrika Mashariki na kuwakutanisha Mondi na Harmonize au Harmo, msanii huyo mpya kwenye muziki wa Kizazi Kipya alifunguka; “Wewe tarajia kuona wasanii wote wakubwa hapa Afrika Mashariki. Kuhusu majina yao nitataja baadaye kadiri siku zinavyokaribia.”

Tanasha alisema kuwa, uzinduzi huo una baraka zote za Mondi ambaye amekuwa akimpa sapoti ya kutosha tangu walipokutana na alipoanza kujiingiza kwenye muziki mwaka jana. Mbali na wimbo huo wa La Vie, mtangazaji huyo wa Radio NGR ya jijini Mombasa, Kenya ameshaachia nyimbo nyingine kama Nah Easy na Radio ambazo zinapatikana ndani ya EP hiyo.

Stori: SIFAEL PAUL, RISASI JUMAMOSI

Leave A Reply