Tanasha; Msanii wa Kuchungwa Sana 2020

BILA shaka utakuwa una taarifa kuwa wimbo bora Afrika Mashariki kwa sasa ni Gere unaomilikiwa na mwanamama mrembo, Tanasha Donna Oketch, akiwa amemshirikisha Diamond Platinumz.

 

Najua hili jina siyo geni sana kwako, lakini kwa kuwa moja ya sifa kubwa za binadamu ni kusahau, ngoja nikukumbushe.

Tanasha Donna, ndiye mpenzi wa sasa wa nyota wa muziki wa Bongo Fleva na mmiliki wa lebo ya WCB, Diamond Platinumz. Tayari wana mtoto mmoja anayeitwa, Nassibu Abdul Junior.

 

Kilichofanya nimlete Tanasha kwenye Kilinge leo siyo kwa sababu ni mpenzi wa staa mkubwa, bali ni kile ambacho amekifanya katika muziki wa Bongo Fleva, kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu.

Kasi kubwa aliyoanza nayo mwaka katika anga za Bongo Fleva imewashangaza wengi.

 

Kabla hatujazungumzia muziki wake na rekodi zake, ni vyema ningekujuza kwa uchache, juu ya wapi katoka na alikuwa anafanya nini kabla sisi hatujamjua kama msanii na mpenzi wa Diamond.

Tanasha ni chotara aliyezaliwa Julai 7, 1996 na baba Muitaliano na mama Mkenya.

 

Akiwa na miaka 11, alikwenda kusoma na kuishi Ubelgiji ambako alisomea mambo ya utalii. Anamudu kuzungumza lugha tano; Kiingereza, Kiswahili, Kiholanzi, Kifaransa na Kihispania.

Alirejea Kenya akiwa na miaka 20, akaanza kujihusisha na mitindo, ambapo pia anamiliki kampuni yake ya nywele, inayoitwa ‘For Her Luxury Hair’, pia ni mtangazaji, aliwahi kutangaza katika kituo cha NRG Radio nchini Kenya.

 

Kwa hapa Tanzania wengi tulimuona kwa mara ya kwanza, baada ya kuwa Video Vixen katika wimbo wa Nagharamia, ulioimbwa na Alikiba pamoja na Christian Bella. Wimbo ukaja ukazua maneno kuwa Kiba anatoka na mrembo huyo, licha ya kuwa wenyewe walikuja kukanusha.

 

Kabla ya kutoka kimapenzi na Diamond, Tanasha alikuwa anatoka na Mkenya, Hunk Nick Mutuma, ambaye ni muigizaji na mtangazaji wa televisheni lakini pia ni mtu wa mitindo, mahusiano ambayo yalidumu kwa miezi sita tu, hiyo ilikuwa ni 2017.

Ilipofika Aprili ndipo zikavuja taarifa kuwa, anatoka na Diamond, mapenzi ambayo yamezaa matunda ya kupata mtoto mmoja.

 

ALIINGIAJE KWENYE MUZIKI?

Kama ilivyo kwa Lulu Diva, Gigy Money, Amber Lulu na wengine wengi kutoka Bongo, ambao walianzia kwenye Uvideo Vixen, Tanasha anasema: “Nilipenda sana muziki tangu nikiwa mdogo, ndiyo maana ikaja kuwa rahisi kwangu kutokea kwenye video za watu nikiwa kama Video Vixen, lakini pia nilijiona nina kipaji cha kweli ndiyo maana nikaanza kufanya muziki baada ya kupata sapoti kutoka kwa Diamond.”

 

AINGIA MZIMA MZIMA KWENYE GEMU

Tanasha ni mmoja wa wasanii ambao wanajua kuzitumia fursa, alipoona kuwa yupo na staa wa muziki Bongo na Afrika, huku penzi lao likiitika mjini, akaamua kuachia ngoma yake ya kwanza, Radio, akimshirikisha Baraka Jaccuzi, ngoma ikitoka Aprili 29, 2019 na ikafanya vizuri ikigonga views (kutazamwa na watu) zaidi ya milioni moja.

 

Hakukaa kizembe, miezi mitatu baadaye akatoa ngoma nyingine, Nah Easy, iliyotoka Julai 10, 2019, ambapo hadi sasa imegonga views zaidi ya laki nane YouTube. Baada ya hapo akatia nukta kwa sababu ya ishu za uzazi, kwa kuwa wakati anashuti Wimbo wa Na Easy alikuwa tayari ni mjamzito.

 

AIANZA 2020 KWA KISHINDO KIKUBWA

Baada ya kuona sasa mwanaye amenyanyuka kidogo, akaamua kuingia studio fasta, kabla hatujakaa sawa, Januari 13 akatupa zawadi nyingine, La Vie, akiwa amemshirikisha Mbosso.

Hapa kidogo watu wakaanza kuwa makini naye na kuona kama vile ana kitu cha utofauti, ikiwa ni wimbo wake wa tatu kutoka, ukafanikiwa kukaa kwenye trending (chati) kwa siku kadhaa, ambapo hadi sasa umegonga zaidi ya views milioni mbili na laki saba.

 

AKADONDOSHA EXTEND PLAY (EP), DONATELLE

Wakati watu wakiwa bado hawajakaa vizuri, Tanasha akaamua kutoa nyimbo nyingi kwa wakati mmoja, ‘Extended Play’(EP) iliyoitwa Donatalle, uzinduzi uliofanyika Nairobi, Kenya.

 

AKATUMALIZA NA GERE

Unaweza kusema ana sifa, baada ya kuona kama vile EP yake inasuasua huko mtandaoni, ndipo akaamua kuunganisha nguvu na baba mtoto wake na kuangusha ngoma ya Gere.

Gere ndiyo ngoma namba moja kwa sasa, ikiwa imetoka Februari 19, hadi sasa ipo namba moja kwa kutrendi katika nchi karibia zote za Afrika Mashariki, uwepo wa Diamond ni moja ya vitu ambavyo vimeipa ukubwa kazi hiyo.

 

Hadi kufikia jana Jumapili video ilikuwa imetazamwa na zaidi ya watu milioni mbili na laki nane, na ikiwa bado ipo kwenye trendi, mashairi matamu, chupa tamu, melodi kali, huku Tanasha akituonyesha uwezo wake wa kucheza na sauti.

 

AWEKA REKODI AFRIKA

Tanasha ameweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa kike kutoka Afrika, kufikisha views milioni moja YouTube, ikiwa video yake haijamaliza hata siku moja.

Tangu Gere, ilipotoka Februari 19, ilichukua takribani saa 14 pekee hadi kufikisha watazamaji milioni moja kwenye mtandao w a YouTube na kumfanya Tanasha aweke rekodi kubwa katika muziki wake.

 

ANABEBWA NA DIAMOND?

Kwa haraka jibu litakuwa ni ndiyo anabebwa na Diamond, lakini hawezi kubebwa kama atakuwa hana kipaji cha kuimba, wote tumemsikia na tumeona anachokifanya, anajua kuimba na hata sauti ipo.


Loading...

Toa comment