The House of Favourite Newspapers

TANASHA WA DIAMOND ALIAMSHA DUDE!

MAMBO ni moto! Baada ya hivi karibuni mrembo kutoka nchini Kenya, Tanasha Donna Barbieri Okech ‘Zahara Zaire’ kuahidiwa ndoa na staa wa Afro Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au Mondi, mwanadada huyo ameamsha dude la aina yake, Risasi Mchanganyiko linakupa mkanda mzima ulivyo.

 

Mara baada ya Diamond kutangaza kwamba atafunga ndoa na mrembo huyo ambaye ni mtangazaji Februari 14, 2019 ambayo ni Siku ya Wapendanao, kumekuwa na manenomaneno mengi huku wengi wakidai kwamba haiwezekani na wengine wakieleza na kufichua mambo mbalimbali yanayomuhusu Tanasha ambaye ndiye mkewe mtarajiwa.

 

Licha ya watu hao ambao ni mashabiki wa Diamond kuzungumza hayo, pia kwa upande wa wale wanawake ambao wamewahi kutoka kimapenzi na staa huyo ’zilipendwa’ nao hawakuwa nyuma kwani kila mmoja amekuwa akiachia ‘bomu’ lake kwa wakati wake, jambo linaloonesha wazi kwamba Tanasha ameliamsha dude ambalo lilikuwa limelala.

 

Uchunguzi wa Risasi Mchanganyiko ulibaini kwamba, zilipendwa hao wana hasira kutokana na kauli zao ambazo nyingine zimezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakilipiza kwa kuonesha wakijiachia na wanaume wengine.

 

MOBETO ATOA POVU

Risasi Mchanganyiko lilimtafuta mzazi mwenzake na Diamond, Hamisa Mobeto ‘Misa’ na kumuuliza maoni yake kwa mke mtarajiwa wa baba mtoto wake huyo ambapo alitoa povu ambalo siyo la nchi hii. “Jamani siwezi na sitaki kuzungumzia uhusiano wa Diamond na hao wanawake zake,” alifoka Hamisa kwa hasira kisha akakata simu.

KIM NANA AIBUKA NA BWANA

Katika kuonesha naye yupo na anaweza kuwa na mwanaume tofauti na jamaa huyo, video queen wa Bongo ambaye hivi karibuni aliyajwa kutoka na Mondi kabla ya Tanasha, Lilian Kessy ‘Kim Nana’ hivi karibuni alionekana kujibu mapigo baada ya kuibuka na bwana mpya huko nchini Kenya alipo kwa sasa.

Picha za Kim Nana na bwana huyo Mkenya zilisambaa mitandaoni hivi karibuni ambapo wataalam wa mambo ya ‘ubuyu’ walisema ameamua kumlipizia Diamond kwani ameenda kuchukua kulekule ambako ametokea mpenzi wa mwanamuziki huyo. Kuna tetesi kuwa mwanaume huyo ambaye Kim Nana anatamba naye amempora kwa video queen matata wa Kenya aitwaye Vera Sidika.

ZARI AMKEJELI DIAMOND

Wikiendi iliyopita Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye naye ni mzazi mwenza wa Diamond alimfanyia mwanaye, Nillan Nasibu ‘Prince’ sherehe ya bethidei ambapo aliweka picha mbalimbali kwenye kurasa tofauti za Mtandao wa Instagram akiwa na watoto wake na watoto wengine wakisherehekea.

 

Wakati akisherehekea huko nchini Afrika Kusini ‘South’ na wanaye huku Bongo, Diamond alipata ajali ya kuanguka jukwaani baada ya jukwaa walilokuwa wakifanyia shoo kudondoka huko mjini Sumbawanga.

Zari alionekana kumkejeli Diamond baada ya shabiki mmoja kumwambia kwenye ukurasa wake aliokuwa ameweka picha za watoto kuwa ana taarifa za baba wa watoto wake huyo kupata ajali ambapo alimjibu kwa kejeli kwamba atamtumia ambulance kutoka Afrika Kusini iende imchukue kwani huko (Sumbawanga) hakuna madaktari! “Subiri nitume ambulance kutoka Sauzi naona unanijulisha hakuna madaktari huko,” alijibu Zari.

 

KINACHOONEKANA

Kinachoonekana kila upande wa zilipendwa wa Diamond umekuwa ukirusha madongo kwa Tanasha ambaye amekuwa akipata wakati mgumu mitandaoni kwa namna anavyoelezewa kuwa hafai kuolewa na Diamond.

DIAMOND ANASEMAJE?

Alipotafutwa Diamond ili kuulizwa kuhusu mambo hayo juzi Jumatatu simu yake iliita bila kupokelewa, lakini alipotafutwa mmoja wa mameneja wangu, Babu Tale alisema walipokuwa wanashusha mizingo kwenye ndege hivyo Diamond atafutwe baadaye. Hata hivyo, alipotafutwa tena simu iliendelea kuita bila kupokelewa huku watu wa karibu wakieleza kuwa alikuwa kwenye maandalizi ya Tamasha la Wasafi Festival visiwani Zanzibar jana.

Stori:Waandishi Wetu, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.