The House of Favourite Newspapers

Tanzania, Kenya Zaondoleana Vikwazo vya Kibiashara

0
Dkt. Augustine Mahiga.

SERIKALI za Tanzania na Kenya zimekubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara zilizokuwa zimewekeana kuhusu bidhaa kutoingizwa katika nchi hizo.

 

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam,  Waziri wa Mambo ya Nje, na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga ameeleza kuwa kuondolewa kwa vikwazo hivyo ni kuzingatia taratibu za kibiashara ambazo zilikubaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Akifafanua, Dkt. Mahiga alisema hatua hiyo itaifanya Kenya kuondoa vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia (LPG) ilivyoviweka dhidi ya Tanzania, na Tanzania kuondoa vikwazo kwa bidhaa za maziwa na sigara zinazozalishwa nchini Kenya.

 

“Juhudi za awali za serikali ya Tanzania ilikuwa ni kuona vikwazo hivyo vinaondolewa na Kenya kwa wakati lakini  hazikuzaa matunda. Hali hiyo ilisababisha Tanzania nayo kuweka vikwazo kwa bidhaa za maziwa na sigara kutoka Kenya zisiingie katika soko la Tanzania,” alisema Mahiga.

 

Alisisitiza kwamba kwa kuzingatia mahusiano mazuri ya kindugu yaliyopo kati ya nchi hizi mbili na kwa kujali manufaa mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, viongozi wakuu wa nchi hizi mbili Dkt. John  Magufuli na Uhuru Kenyatta wa Kenya walikubaliana kuviondoa vikwazo hivyo mara moja.

 

Hatua hiyo ya kuondoa vikwazo hivyo ilifuatia maelekezo waliyotoa viongozi hao kwa mawaziri wao wa mambo ya nje, Dkt. Augustine Mahiga na Dkt. Amina Mohammed wa Kenya.

NA DENIS MTIMA | GPL

 

INSTALL GLOBAL PUBLISHERS APP sasa usipitwe na matukio
PAKUA HAPA==>GLOBAL PUBLISHERS APP

FULL VIDEO; Mapambano Ngumi za Global TV – Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania Bingwa

Leave A Reply