The House of Favourite Newspapers

TANZANIA KUKUMBUKA WALIOKUFA VITA YA DUNIA

TANZANIA inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 100 ya Mashujaa waliokufa kwenye Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914 hadi 1918. Vita hiyo ambayo kwa sehemu kubwa ilihusisha makoloni mawili ya Wajerumani kwa upande mmoja na Waingereza kwa upande mwingine, iliwatumia askari wa Afrika waliopewa mafunzo ya kijeshi na wakoloni hao.

Katibu wa Klabu ijulikanayo kama ‘British Legion Tanganyika Club’, David Sawe, aliliambia gazeti hili jana kwa njia ya simu kuwa, maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika kwenye makaburi ya mashujaa hao yaliyopo Makumbusho Kijitonyama jijini Dar es Salaam kuanzia saa mbili asubuhi.

Sawe alisema maandalizi ya maadhimisho hayo kwa sehemu kubwa yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Ujerumani na Uingereza zilizopo nchini. Alisema miongoni mwa shughuli zitakazofanyika wakati wa maadhimisho hayo ni gwaride la heshima kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), sala itakayoandaliwa na Ubalozi wa Uingereza kwa kushirikisha madhehebu mbalimbali ya dini.

Aliyataja madhehebu hayo kuwa ni Anglikana, Katoliki, Waislamu, Walutheri na kisha kufuatiwa na sala itakayosimamiwa na Ubalozi wa Ujerumani, ambayo madhehebu ya Kilutheri ndiyo yatakayohusika kuongoza sala hiyo.

“Wakati wa vita hivyo, Tanganyika ilipigana pande zote mbili, upande wa Wajerumani na upande wa Waingereza. Wajerumani waliwatumia askari wa Kiafrika kutoka Tanganyika, Burundi na Msumbiji, wakati Waingereza waliwatumia askari wa kiafrika kutoka Kenya, Afrika Kusini, Cameroon na India,” alieleza Sawe.

Kwa mujibu wake, vita hivyo vilianza kwa Wajerumani kuanza kuwashamabulia Waingereza, lakini baadaye Waingereza walijipanga na kuendesha mapambano hadi Tanganyika kupitia Tanga na Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema Waingereza walifanikiwa kuwasukuma Wajerumani kuelekea kusini hadi walipokimbilia nchini Msumbiji na kuongeza kuwa wakati huohuo Waingereza walikuwa wakitoa mafunzo ya kijeshi kwa wananchi wa Tanganyika pamoja na wabeba mizigo, lakini pia askari wa waliotekwa waliokuwa wakitumiwa na Wajerumani, baadaye walitumiwa na Waingereza katika kupigana dhidi ya Wajerumani.

“Baada ya kufika Msumbiji, Wajerumani waliteka silaha za Wareno kwa kuwa Jeshi la Wareno halikuwa imara sana, mara baada ya kuziteka silaha hizo walijipanga kurudi kupambana na Waingereza, walipokuwa mji wa Mbala kujiandaa kuwapiga Waingereza, ndipo walipopata taarifa ya kumalizika kwa vita,” alieleza veterani huyo.

Alisema mkataba wa kumaliza vita hivyo vya Kwanza vya Dunia ulisainiwa Novemba 11, 1918 huko Ulaya na ilipofika Novemba 25, mwaka huohuo, Wajerumani walisalimu amri na kukabidhi silaha kwa Waingereza huko Mbala. Kwa mujibu wa Sawe, Waingereza na Wajerumani walikuwa hawaweki kumbukumbu vizuri ya askari wa Kiafrika waliokufa kwenye vita hivyo, bali walikuwa wanaweka kumbukumbu ya maofisa wao zaidi. Alisema baadhi ya makaburi ya mashujaa hao pia yapo Kinondoni na Upanga jijini Dar es Salaam.

Chanzo:  Mwananchi

 

Comments are closed.