The House of Favourite Newspapers

Tanzania Kuwa Mwenyeji wa Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki (11TH East African Petroleum Conference and Exhibition – EAPCE25), utakaofanyika tarehe 5 hadi 7 Machi 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Kauli mbiu ya Mkutano huu, ni Kufungua Fursa za Uwekezaji katika Nishati: Mchango wa Rasilimali za Mafuta katika Kupata Nishati ya Uhakika kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika Mashariki, Mkutano huu utafunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huu utatanguliwa na semina kuhusu masuala ya nishati safi ikiwemo nishati safi ya kupikia na matumizi ya gesi kwenye magari (CNG) itakayofanyika tarehe 4 Machi, 2025.
Mkutano wa EAPCE25 utawaleta pamoja washiriki zaidi ya 1000, wakiwemo watunga sera, viongozi wa Serikali kutoka nchi mbalimbali ikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wawekezaji wa kimataifa na wa ndani.
Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba alisema kuwa Mkutano huu wa EAPCE25 utatoa nafasi ya kujadili mchango wa rasilimali za mafuta na gesi asilia katika mchanganyiko wa nishati kwa maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi Afrika Mashariki”.
 Aidha, Mhandisi Mramba alieleza kuwa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam na wabobezi katika sekta ya mafuta na gesi zitatolewa zikiwemo utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi katika nchi za Afrika Mashariki, fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi, dhana ya kuelekea nishati safi, masuala ya mazingira, miundo ya kisera, kisheria na kiudhibiti katika mafuta na gesi na kadhalika.
Vilevile, mkutano utahusisha maonesho ya bidhaa na huduma kutoka kampuni mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia.
Aidha, Mhandisi Mramba alieleza kuwa Mkutano wa EAPCE25 unafanyika katika wakati muhimu baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kujadili masuala ya nishati.