The House of Favourite Newspapers

Tanzania mojawapo ya nchi 10 zisizo na furaha duniani

0

tanzania_flag_map

TANZANIA ni miongoni mwa nchi kumi za mwisho kwa viwango vya furaha kwa mujibu wa Ripoti ya Viwango vya Furaha Duniani ya 2016 ambayo imetolewa jana.

Orodha hiyo iliyoandaliwa kwa kuangazia pato la mtu kwa kila mwaka, miaka ambayo mtu anatarajiwa kuishi, kuwa na mtu wa kutegemea kwa usaidizi, dhana ya kuwepo uhuru wa kufanya maamuzi maishani, uhuru kutoka kwa ufisadi, na ukarimu miongoni mwa mengine.

Large-group-of-young-people-enjoying-a-beach-party_147047612

Mataifa yaliyo kwenye kundi la mataifa kumi ya mwisho ni Madagascar, Tanzania, Liberia, Guinea, Rwanda, Benin, Afghanistan, Togo, Syria huku Burundi ikishika mkia.

Tanzania ipo nambari 149 kati ya nchi 157 ikiwa na alama 3.695 kati ya alama 10 na Rwanda nambari 152 na alama 3.315.

Uganda ipo nambari 146 na alama 3.739, Malawi nambari 132 na alama 4.156, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ipo nambari 125 na alama 4.272 na Kenya nambari 122 na alama 4.356.

Somalia ipo nambari 76 na alama 5.44.

Ripoti hiyo imetolewa mjini Roma, Italia huku ulimwengu ukijiandaa kuadhimisha Siku ya Furaha Duniani ya Umoja wa Mataifa tarehe 20 Machi.

Orodha hiyo imetayarishwa na shirika la maendeleo endelevu ya Sustainable Development Solutions Network (SDSN) ambalo lilianzishwa na Umoja wa Mataifa.

Denmark inaongoza kwa viwango vya furaha duniani ikiwa na alama 7.526 ikifuatwa kwa karibu na Uswizi, Iceland na Norway.

Finland, Canada, Uholanzi, New Zealand, Australia na Sweden zinafunga kumi bora.

Marekani ipo nambari 13 na Uingereza nambari 23.

Credit: BBC

Leave A Reply