Tanzania Na Indonesia Kushirikiana Katika Udhibiti Wa Dawa
Tanzania na Indonesia zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya usajili, ukaguzi na udhibiti wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitandanishi.
Hafla ya utiaji saini wa hati ambayo imeshuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi imefanyika leo tarehe 03 Septemba 2024 jijini Bali, Indonesia pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika.
Kwa upande wa Tanzania, hati hiyo imesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi Tanzania, Dkt. Adam Fimbo na Serikali ya Indonesia iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Chakula, Dkt. Taruna Ikrar.
Aidha, wakati wa hafla hiyo Mhe. Rais Mwinyi aliongozana na Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Amina Khamis Shaaban na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Tembele.
Kusainiwa kwa hati hii kutaziwezesha nchi hizi kushirikiana kwa karibu katika masuala yote yanayohusu ukaguzi, udhibiti, usajili wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi huku msisitizo ukiwekwa kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kutekeleza jukumu hilo.
Wakati huohuo, Tanzania na Indonesia zimebadilishana Hati ya Makubaliano ambayo ilisainiwa na nchi hizi mbili mwezi Agosti 2024 kuhusu ushirikiano katika masuala ya mafuta na gesi kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Serikali ya Indonesia ya PERTAMINA. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue aliiwakilisha Tanzania kwenye hafla ya kubadilishana hati hiyo na Indonesia iliwakilishwa na Ibu Nicke Widyawati, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Pertamina.