Tanzania na Urusi Kushirikiana Kuendeleza Utalii
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekubaliana kushirikiana na Nchi ya Urusi katika kukuza na kuendeleza Sekta ya Utalii.
Hayo yamebainika leo Oktoba 28,2024 katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) na ujumbe kutoka Urusi ulioongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Kiuchumi nchini Urusi, Mhe. Maxim Gennadyevich Reshetnikov, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe.Chana amesema Tanzania na Urusi imekuwa na mahusiano ya muda mrefu tangu mwaka 1961 na zimekuwa zikishirikiana katika masuala mengi ikiwemo uchumi, diplomasi na mambo ya kijamii.
Kupitia kikao hicho Tanzania na Urusi zimekubaliana kuboresha mashirikiano yatakayokuza utalii baina ya nchi hizo mbili ikiwemo programu za elimu ya utalii (Chuo kikuu cha Urusi na Chuo cha Taifa cha Utalii), Utangazaji Utalii wa pamoja katika Maonesho ya Kimataifa, Bodi za Utalii na Makumbusho za Taifa za nchi hizo mbili kubadilishana uzoefu, pamoja na uendelezaji wa vitega uchumi hasa katika mahoteli ya kitalii nchini ili kuvutia idadi kubwa ya watalii kutoka nchini Urusi.
Aidha, wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya usafiri wa anga na kurahisisha mfumo wa malipo kwa watalii wanaotembelea nchini Tanzania ili waweze kutumia kadi za Urusi.
Naye, Mhe. Maxim Gennadyevich Reshetnikov amesema sababu ya kuichagua Tanzania ni kutokana na sifa yake ya kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo mbuga za Wanyama na Mlima Kilimanjaro huku akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi nzuri ya kuendeleza utalii.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi,Mkurugenzi wa Bodi Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru, Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt.Noel Luoga na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.