The House of Favourite Newspapers

Tanzania ya Magufuli inaweza kusimamia bajeti bila wahisani

0

71d6pombeRais wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.

Kasi aliyoingia nayo madarakani Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli imeendelea kuwa gumzo kila kona, ndani na nje ya nchi huku wadau wengi wakionesha kumpongeza hasa katika suala zima la kuhakikisha serikali yake inakusanya kodi kwa wingi na kuziba mianya yote ya ‘upigaji’ wa mali za umma uliokuwa umekithiri.

Ipo wazi kwamba mataifa yote makubwa yaliyoendelea duniani, ikiwemo Marekani na nchi nyingine za Ulaya, hutegemea kwa kiasi kikubwa makusanyo ya kodi kutoka kwa wafanyabiashara, kuanzia wale wakubwa mpaka wadogo kabisa.

Kwa wenzetu, kila mwananchi anapofanya shughuli yoyote ya kumuingizia kipato, lazima alipe kodi inayostahili. Huenda ikaonekana kama maajabu lakini kwa nchi kama Marekani kwa mfano, kuanzia wasanii wa muziki na filamu, wacheza soka, wafanyabiashara, wanamitindo, mabondia na wengine wengi, wanalipa kodi kila kukicha.

Kwa kutumia kodi tu, Marekani imeweza kujenga uchumi imara duniani na kuifanya iheshimike na kila mmoja. Kwa kipindi kirefu, hali ilikuwa tofauti kabisa kwa Tanzania, nchi tajiri iliyojaliwa kuwa na rasilimali kedekede, kuanzia mbuga za wanyama, madini ya kila aina kama dhahabu, almasi, urani (Uranium) na Tanzanite ambayo haipatikani sehemu nyingine yoyote duniani zaidi ya Tanzania.

Unaweza kujiuliza ni nini kimekuwa kikiikwamisha Tanzania kupiga hatua ya kuondokana na umaskini kwa kipindi kirefu, ikiwa ni tayari nusu karne imepita tangu kupatikana kwa uhuru kutoka kwa wakoloni.

Viongozi wa juu wa nchi, akiwemo aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete na aliyekuwa waziri mkuu wake, Mizengo Pinda, kwa nyakaati tofauti wamewahi kunukuliwa wakisema hata wao hawajui ni kwa nini Watanzania ni maskini wakati nchi yao imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi.

Kwa kipindi kifupi tu tangu alipoingia madarakani, Rais Magufuli ameonesha njia na tayari Watanzania wengi waliokuwa wamekata tamaa na kupoteza uzalendo ndani ya mioyo yao, wameanza kuamini kwamba kumbe mabadiliko ya kweli yanawezekana.

kifanya utafiti mwepesi mitaani, utaona kwamba Watanzania wengi wana matumaini ya kuondokana na umaskini katika kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote.

Kwa kutambua umuhimu wa kodi, Rais Magufuli ameamua kuelekeza nguvu zake kwenye eneo hilo kwanza kwa kuhakikisha watu wote wanalipa kodi halali na kuachana na ujanjaujanja uliodumaza uchumi wa taifa kwa kipindi kirefu sasa.

Ipo dhahiri kwamba Magufuli akiendelea na moto huu, miaka mitano ijayo tutakuwa tukiizungumzia Tanzania tofauti kabisa na huenda nchi yetu ikawa mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia nzima kwa jumla.

Ni aibu kwa bajeti ya serikali kutegemea wahisani wakati kila kitu tunacho hapa nchini. Katika bajeti ya serikali ya mwaka 2014/2015, serikali ilipitisha bajeti ya shilingi trilioni 19.6, ikiwa ni ongezeko kutoka trilioni 18.2 kwa kipindi cha mwaka 2013/ 2014.

Mwaka huu wa fedha wa 2015/2016, serikali imepitisha jumla ya shilingi trilioni 22 katika bajeti ya serikali, huku sehemu kubwa ikionesha kuwa bado tunategemea wahisani katika kupatikana kwa fedha hizo za bajeti. Wakati huohuo, deni la taifa mpaka kufikia Machi, 2015 lilikuwa limepaa na kufikia shilingi trilioni 35.

Huhitaji kuwa msomi wa chuo kikuu kuchambua takwimu hizo na kuona jinsi nchi ilivyokuwa ‘ikipumulia mashine’ kiuchumi, huku rasilimali za taifa zikiendelea kuwanufaisha wachache na mamilioni ya Watanzania wakiendelea kuishi chini ya dola moja kwa siku.

Narudia kusisitiza tena, Magufuli akiendelea na kasi hii, itafikia kipindi ambapo Tanzania itaweza kujitegemea katika bajeti yake bila kuhitaji misaada kutoka kwa wahisani kwa sababu tayari Mungu ameijalia nchi yetu kuwa na kila kitu.

ilichotufikisha hapa ni kukosa usimamizi bora, ujasiri wa watawala wa nchi na uthubutu kama alionao Magufuli.
Mungu ibariki Tanzania.

Leave A Reply