The House of Favourite Newspapers

Tanzania ya Magufuli iwe Tanzania ya Watanzania

0

Rais Magufuli (11)Rais Dk.John Magufuli akisalimia wagonjwa Hospitali ya muhimbili jana.

MAGEUZI ya kuondoa mfumo wa kinyonyaji ni vita ambayo mtu mmoja hawezi kushinda.

Haya ndiyo mapambano aliyoyaanza Rais Dk.John Magufuli aliyelenga kuleta mabadiliko ya uchumi wa nchi.

Siku tatu tangu aingie madarakani Dk. Magufuli, amewaambia watendaji wakuu wa serikali waache uzembe,ufisadi na wakusanye kodi kwa uaminifu huku akisisitiza wafanyabiashara wakubwa wabanwe zaidi ya mama lishe.

Ziara ya kushtukiza aliyoifanya Wizara ya Fedha na kujionea utoro wa baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo nyeti pamoja na kupiga marufuku ziara za nje za maofisa wa serikali zisizokuwa na tija; ni mwanzo mzuri wa usimamizi wa rasilimali za taifa.

Maandiko matakatifu katika Biblia; Yohana 10.32 yanasema: Yesu akawajibu, kazi njema nyingi nimewaonesha zitokazo kwa baba, kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?

Katika maandiko hayo Mtume Yesu analalamika kupigwa mawe kwa kazi njema alizowafanyia watu, kuwaponya na kuwapa chakula.

Nasherehesha; pamoja na mema ambayo Rais Magufuli amedhamiria kuwafanyia wananchi wanyonge bado naliona genge la watumishi waliozoea kutukuzwa na kunyonya mali za umma wataanza kumpiga kwa mawe. Sifikirii wafanyabishara wakubwa waliokuwa wakikwepa kodi, watendaji mafisadi waliotumia vyeo vyao kujineemesha, watamfurahia Rais Magufuli aliyekuja na zege la kuziba ufisadi wao.

Historia inaonesha mapambano ya kuwakomboa wanyonge hujenga uadui baina ya wanyonyaji wachache dhidi ya wanyonywaji wengi!

Kama ilivyokuwa katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni wavamizi wa Bara la Afrika ambapo wapigania uhuru mbalimbali akiwemo Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere walivyojitolea na kuungwa mkono na wananchi ndivyo Rais Magufuli ameamua kulinusuru taifa hili na wakoloni mamboleo hivyo naye hana budi kuungwa mkono na umma.

Katika nchi hii pamoja na uhuru wa bendera tulionao; kama taifa bado nchi iko kwenye utumwa wa umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi wa kutisha ambao unaletwa na kundi la watu wachache walioamua kujimilikisha uchumi wa nchi kwa masilahi yao.

Kwa kutambua hilo, Tanzania ya Magufuli inayojengwa na rais huyu lazima iwe Tanzania ya Watanzania wote ili lengo hili la kuleta mabadiliko lisikwamishwe na mafisadi wachache.

Kama ilivyokuwa enzi za mitume na wapigania ukombozi wengine; wanyonyaji huwa hawako tayari kuachia mkate wao utiwe mchanga.

Mara zote huandaa hila kwa lengo la kuwafitinisha waleta mabadiliko ya kweli dhidi ya umma ili wanyonyaji wasinyang’anywe tonge, jicho la tatu linanionesha hata Rais Magufuli anaweza kufanyiwa hivi.

Napenda kuuambia umma unaofurahia mwanzo mzuri wa uongozi wa Rais Magufuli unalo jukumu zito nyuma ya kiongozi huyo kuhakikisha kuwa unampa nguvu ya kumuwezesha kutimiza ndoto ya ujenzi wa Tanzania mpya.

Rais Magufuli asipoungwa mkono, kazi yake itahujumiwa na mafisadi, hawa ndiyo watakaoandaa maandamano na migomo ya hapa na pale kuhalalisha unyonyaji wao.

Watu wa aina hii wamo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Magufuli na hata nje ya chama hicho tawala.

Lazima jamii hii ifahamu kuwa, utawala wa rais huyu mpya wa awamu ya tano ni vita kati ya wanyonyaji wazoefu wachache wa nchi hii dhidi ya wanyonywaji wengi ambao ni raia wa kawaida. Pamoja na kwamba siwezi kuwa mdhamini wa utendaji wa Rais Magufuli katika awamu hii lakini itoshe kumuunga mkono katika hatua hii nzuri aliyoanza nayo.

Namalizia kusema, bila kujali itikadi za vyama; Watanzania hawana budi kuungana katika kupigania ustawi wa taifa na kuleta mabadiliko ya kweli ya uchumi uliodorora kwa miaka mingi. Muda wa siasa umepita!

Leave A Reply