testiingg
The House of Favourite Newspapers

Tanzania Yashiriki Maonesho ya Kimataifa ya Japan Tourism Expo

0

Tanzania imeshiriki kwa mafanikio makubwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyoanza Oktoba 26, 2023 jijini Osaka, Japan.

Maonesho haya, yamekuwa ya kwanza kufanyika katika jiji hilo baada ya janga la UVIKO – 19 ambapo yalihitimishwa Oktoba 29, 2023 huku takriban makampuni ya watalii 1,275 kutoka nchi zipatazo 70 duniani yakishiriki.

Pamoja na mambo mengine, Tanzania imepata fursa ya kuzindua rasmi filamu ya The Tanzania Royal Tour jijini Osaka ambayo imetafsiriwa kwa  lugha ya Kijapani, tukio ambalo limepata muitikio mkubwa na hamasa kubwa  miongoni mwa Wajapani wanaoishi katika jiji hilo na majiji jirani, ambapo  tukio kama hilo lilifanyika mwaka jana jijini Tokyo.

Taasisi za utalii za Tanzania zilizoshiriki katika maonesho hayo ni Bodi ya  Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),  Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na makampuni binafsi ya utalii  ya Tanzania yakiwemo, GOSHEN Afrika Safari na MAULY Tours.

Maonesho yalilenga kuwavutia Wajapani wengi kutembelea Tanzania  hususan, baada ya Serikali ya Japan kufungua mipaka yake hivi karibuni  kufuatia kupungua kwa janga la UVIKO-19.

Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia  Suluhu Hassan imelenga kukuza uchumi wa nchi kupitia utalii ili hatimaye kufikia watalii milioni 5 na mapato bilioni 6a kwa mwaka 2025.

Mawakala wa utalii Japan wamekuwa wakivutiwa na vivutio vya utalii vya Tanzania pamoja  na uwekezaji katika sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuingia ubia na  makampuni ya utalii ya ndani.

Katika ufunguzi wa Maonesho hayo, Balozi Baraka Luvanda anayeiwakilisha Tanzania nchini Japan, alitoa wasilisho maalum kwa mawakala wa utalii wa Japan waliojumuika na mawakala wa Tanzania ambapo, aliinadi Tanzania na vivutio vyake.

Aidha, Balozi Luvanda alifanya mazungumzo na Kamishna wa Taasisi ya Utalii ya Japan kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta ya utalii.

Vilevile, Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuelezea Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Swahili (Swahili Internation Tourism Expo – S!TE) ya mwaka 2024 yatakayofanyika mwezi Oktoba 2024, kwa wadau mbalimbali wa utalii  wa Japan kwa kuwahamasisha kujiandikisha ili waweze kushiriki kwa lengo la kuunganisha mawakala wa utalii wa Tanzania na Japan, kibiashara.

Japan ni soko linalochipukia (emerging market) baada ya janga la UVIKO – 19 na ni nchi yenye watu takriban milioni 123 ambapo, inaelezwa kuwa watu takriban milioni 23 sawa na asilimia 45 wana tabia ya kutoka kwenda kutalii nje ya nchi.

 

Leave A Reply