
SERIKALI ya Tanzania leo Jumatano, Oktoba 27, 2021 imetoa leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini kwa kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited.
Hafla ya utoaji leseni pia imeenda sambamba na uzinduzi wa taarifa ya uhamasishaji, uwazi na uwajibikaji katika rasilimali madini, mafuta na gesi asilia.
Akzungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Madini Dotto Biteko, amesema uwekezaji huu mbali na kuongeza pato la taifa lakini pia utazalisha ajira. Kazi hii kubwa imefanywa na Timu ya majadiliano ambayo imechangia kufikia kwa utoaji wa leseni hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Tanzania kutoa leseni kubwa ya uchimbaji wa Nickel. Mara ya mwisho kutolewa kwa leseni ya aina hii ilikuwa ni mwaka 2015, ambapo mpaka sasa utekelezaji wake haujaanza.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, Job Ndugai amepongeza hatua hiyo na kusema amefurahi kuona utoaji leseni umefanyika hadharani tofauti na ilivyokuwa katika mikataba mengine.

