The House of Favourite Newspapers

Tanzania Yawa ya Pili Kombe la Dunia Watoto wa Mitaani Urusi (Picha + Video)

Mchezaji wa Tanzania akiwa na kombe la nafasi ya pili la michuano ya kombe la dunia la Watoto wa Mitaani.

Mashindano ya Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani chini ya shirika la Street Child United na udhamini wa makampuni,  taasisi tofauti na kampuni ya mawasiliano ya simu ya nchini Urusi, Megafon, yamefikia tamati jana kwa kuchezwa mechi za mshindi wa tatu na fainali kwa wanawake na kwa wanaume.

Mshindi wa tatu kwa wanawake ni Uingereza baada ya kuifunga Ufilipino magoli 2-0 na kwa wanaume ni Burundi baada ya kuibwaga Indonesia magoli 3-1.

Fainali kwa wanawake ilikuwa Tanzania na Brazil ambapo Brazil iliifunga Tanzania 1-0. Goli hilo lilifungwa mwisho wa kipindi cha kwanza baada ya kutokea mawasiliano mabaya kati ya mlinzi wa Tanzania na mlinda mlango wake. Mchezo huo pia ulikuwa ni wa aina yake, wa kasi na wa kutafutana makosa kwa kila timu.

 

Tanzania ilikuwa na nafasi za kufunga kipindi cha kwanza lakini haikufanya vizuri katika umaliziaji. Brazil walimiliki mchezo zaidi na hasa viungo wao walimficha kiungo mkuu wa Tanzania, nahodha Asteria Robert. Kipindi cha pili Tanzania kidogo walicheza vizuri lakini hawakurudisha goli hilo.

Timu ya wanawake ya Tanzania wakipozi mbele ya kamera.

Kipindi cha kwanza Tanzania walicheza kwa presha kubwa  na hawakutulia na mpira, hali iliiyowaondolea kujiamini. Lakini mwisho wa siku Tanzania ikashika nafasi ya pili katika mashindano hayo kwa wanawake.

Kwa upande mwengine mechi hio ya fainali ilihudhuriwa na watu wengi mashuhuri wakiwemo maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Urusi.

Mmoja wao ni mchezaji wa zamani wa Arsenal na bingwa wa Kombe la Dunia kwa kikosi cha Brazil na kiungo maarufu duniani, Gilberto Da Silva.

 

Kiungo huyu aliichezea Brazil na alishinda Dombe la Dunia mwaka 2012,  na alishinda kombe la ligi kuu ya Uingereza na Arsenal na pia alichezea klabu ya Olimpiakos ya Ugiriki na pia alishawahi kushinda kombe la Copa America akiwa na Brazil na kombe la klabu bingwa barani Amerika ya Kusini au Copa Liberatadores.  Timu zote baada ya mechi zilipata nafasi ya kumuuliza swali moja Gilberto Da Silva.

Tanzania iliuliza swali kupitia nahodha wake, Asteria Robert,  kwa Kiswahili na mkalimani Mohamed Masour Nassor akatafsiri moja kwa moja kwa lugha ya Kireno ya mchezaji huyo. Swali hilo lilikuwa: “Je,  ni vipi unawasaidia watoto wa mitaani kufikia ndoto zao na wale watoto ambao wanataka kuwa wachezaji wa viwango vya dunia kama wewe?”

Mwisho ikafuata sherehe ya ufungaji wa mashindano hayo. Wageni mashuhuri wengi walikuwepo,  wakiwemo Rais wa Chama cha Mpira cha Urusi, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni iliyodhamini michezo hiy,  Megafon,  na shirika la Street Child United kutoka Uingereza,

Mabalozi mbalimbali walikuwepo wa Kombe la Dunia la mwaka 2018 litakalofanyika nchini Urusi, Mkurugenzi wa Masuala ya Jamii  na Utamaduni wa Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba, wachezaji wa zamani wa Urusi na mwandishi wa gazeti la michezo la Urusi kutoka mji wa Saint Petersburg, na wengine.

Kepteni wa timu ya Tanzania akitoa neno la shukurani kwa watayarishaji wa michezo hiyo.

Muda wa zawadi ulipofika, Tanzania ilizawadiwa kombe na medali za shaba kwa kila mchezaji  zilizotolewa na viongozi wa timu kutoka chama cha mpira cha Urusi na zawadi nyingine kutoka kwa chuo cha Patrice Lumumba. Tanzania pia ilitoa kiungo bora wa mashindano ambaye ni nahodha, Asteria Robert. Kwa upande wa mabingwa wa wanaume , ni timu ya Uzbekistan iliyoil€ kwa mikwaju ya penati timu ya Pakistan.

Kwa upande wa zawadi nyngine, mlinda mlango bora alitoka Uingereza kwa wanawake, kwa wanaume alitoka Indonesia, Mfungaji bora kwa wanawake alitoka Brazil, mlinzi bora kwa wanawake pi alitoka Ufilipino,  ambapo mlinzi bora kwa wanaume alitoka Uzbekistan, mchezaji bora kwa wanaume akitoka Pakistan, na mchezaji bora kwa wanawake alitoka Brazil.

Mashindano hayo yalifikia tamati huku yakiwa yameleta faida kubwa katika mpira kama mashindano lakini pia kujuana kwa watoto hawa wa dunia nzima na pia kufanya utalii sehemu mbalimbali za mji wa Moscow na kujifunza mambo mengi.

Manufaa mengine ni mikutano ya watoto kutoka nchini mbalimbali ambako walipewa nafasi ya kutoa  mawazo na changamoto zao na kupata hadi za misaada mbalimbali. Nchi zilizoshiriki ni 21 na timu zikiwa ni 24. Tanzania kwa ujumla imeweka rekodi nzuri kwa kuwa mshindi wa pili mwaka huu kwa wanawake.

 

Mwaka 2014 Tanzania ilikuea bingwa wa mashindano haya kwa wanaume huko Rio de Janeiro, Brazil,  na mwaka 2010 Tanzania iliishia nusu fainali huko Afrika Kusini kwa upande wa wanaume.

Michuano mingine kama hiyo itafanyika mwaka 2022 nchini Qatar,  ambapo Tanzania inatazamiwa kufanya vizuri zaidi.

Stori na Mohamed Mansour Nassor
SOYUZ Alumni Association of Tanzania

Comments are closed.