The House of Favourite Newspapers

TANZIA: Kocha wa Mwadui FC Afariki Dunia

Kocha msaidizi wa Mwadui FC inayoshiriki Ligi kuu Tanzania Bara, Jumanne Ntambi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Januari 24.

 

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeeleza kuwa kocha huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu.

Imeelezwa kuwa tatizo hilo lilimfanya kushindwa kuhudhuria mazoezi ya Mwadui yaliyofanyika jana na badala yake alifika mazoezini mwishoni kabla ya usiku mauti kumkuta akiwa nyumbani kwake, mkoani Shinyanga.

Kocha huyo alikuwepo kwenye benchi la ufundi la timu hiyo katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania

Bara zilizopita, ukiwemo ule uliopigwa kwenye dimba la Uhuru Dar es Salaam dhidi ya Yanga uliomalizika kwa suluhu na wa mwisho ulikuwa ni dhidi ya Ndanda FC uliopigwa Jumapili iliyopita na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye dimba la Mwadui Complex, Shinyanga.

 

Enzi za uhai wake Ntambi aliwahi kufundisha Timu za Kahama United ya Shinyanga, Mlale JKT ya Ruvuma, Panone ya Kilimanjaro, Timu ya Mkoa wa Shinyanga, Igembe Nsabo na mpaka mauti yanamkuta alikuwa akiifundisha Mwadui ya Shinyanga akiwa kocha msaidizi.

 

Kufutia msiba huo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na familia ya wanasoka kwa jumla nchini Tanzania.

“Kifo cha Kocha Ntambi kimenishtua mno na kwa niaba ya shirikisho natoa pole kwa wafiwa nawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu kwao kumpoteza mpendwa wao, hakika alikuwa kocha aliyejitahidi kuibua vipaji na amekuwa na mchango mkubwa katika mpira wa miguu ambao bado alikuwa anautumikia mpaka kifo chake,” amesema Rais Karia.

Nabii Tito Mbaroni, Abainika na Ugonjwa wa Akili

Comments are closed.