Tanzia: Dkt. Makongoro Mahanga Afariki Dunia

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kichama wa Ilala Jijini Dar es Salaam, Dkt. Milton Makongoro Mahanga,  amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Machi 23, 2020 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu tangu juzi.

 

Katibu wa Chadema Mkoa wa Ilala, Jerome Olomi, amethibitisha kutokea kwa msiba huo na kusema taarifa zaidi kuhusu msiba huo zitatolewa baadaye.

“Habari makamanda, taarifa mbaya tusizozitegemea tulizozipata asubuhi hii mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ilala Dr Milton Makongoro Mahanga  amefariki dunia. Tutazidi kupeana taarifa za taratibu nyingine,” inaeleza taarifa ya Olomi.

Olomi amesema Chadema inaendelea kuwasiliana na ndugu wa marehemu kwa ajili ya kujua taratibu za mazishi, kisha kitatoa taarifa baadaye kuhusu msiba huo.

Dk. Makongoro kabla umauti kumfika alikuwa Mwenyekiti wa Chadema wilayani Ilala, awali alikuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Ukonga kisha Segerea.

 

Pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Naibu Waziri wa Miundombinu na Maendeleo, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa nyakati tofauti wakati akiwa mbunge katika serikali ya awamu ya nne, chini ya Rais Mstaafu, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kabla kuhamia Chadema. 

 
Toa comment