Kartra

Tanzia: Mbowe Apata Pigo, Baba Yake Mdogo Afariki Dunia

MZEE Manase Alphayo Mbowe, baba mdogo wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amefariki dunia asubuhi ya leo Ijumaa Julai 23, 2021 Hospitali ya Machame alikokuwa akipatiwa matibabu. Hayo yamethibitishwa na James Mbowe, mtoto wa Freeman.

 

MANASE Alphayo Mbowe, baba mdogo wa Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe, amefariki dunia asubuhi ya leo Ijumaa, Julai 23, 2021 katika Hospitali ya Machame mkoani Kilimanjaro, alikokuwa anapatiwa matibabu.

 

Taarifa ya kifo hicho imetolewa leo Ijumaa na James, mtoto wa Freeman ambaye amesema Mzee Mbowe, alishtushwa baada ya kusikia tuhuma za kupanga njama za ugaidi zinazomkabili mwanae.

James amesema, babu yake huyo alifariki dunia akipatiwa msaada wa kupumua kwa kutumia mashine ya oksijeni, hospitalini hapo lakini “Leo asubuhi akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo amefariki dunia.”

 

James amesema, taratibu za mazishi yake zitatangazwa baadae baada ya familia kukutana. Amesema, enzi za uhai wake, babu yake huyo aliwahi kufanya kazi serikalini ikiwemo ofisi ya Rais. Ameacha watoto watano, wa kike mmoja na wa kiume wanne.

 

Kifo hicho ni pigo jingine kwa Mbowe ambaye tangu usiku wa kuamkia juzi Jumatano tarehe 21 Julai 2021, amekuwa mikononi mwa jeshi la polisi. Mbowe na wenzake 11, walikamatwa wakiwa katika Hotel ya Kingdom jijini Mwanza, walipokwenda kwa ajili ya kufanya kongamano la kudai katiba mpya.

 

Hata hivyo, kongamano hilo halikufanyika kutokana na kutiwa mbaroni. Wakati wenzake 11 wakibaki Mwanza, Mbowe alisafirishwa hadi Dar es Salaam ambapo polisi walikwenda kufanya upekunzi nyumbani kwake, Mikocheni. Na jana Alhamisi, Jeshi la Polisi Tanzania lilisema linamshikiliwa mbowe kwa tuhuma za kupanga njama za mauaji ya viongozi wa serikali na ugaidi.

 

Huu ni msiba wa pili kumkuta Mbowe ndani ya wiki chache, baada ya kaka yake, Charles Mbowe, kufariki dunia, tarehe 8 Julai 2021, na mwili wake kuzikwa nyumbani kwao Machame mkoani Kilimanjaro, tarehe 12 Julai 2021.


Toa comment