
MWANDISHI wa habari, Douglas David, amekutwa amefariki dunia chumbani kwake eneo la Vingunguti Mji Mpya, jijini Dar es Salaam, huku mwili wake ukiwa umeharibika vibaya jana Jumatatu Januari 27, 2020.
Inaelezwa kuwa Douglas aligunduliwa na majirani zake baada ya kuhisi harufu kali kutoka chumbani kwake, ndipo wakafanya utaratibu wa kufungua mlango kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya mtaa chini ya usimamizi wa polisi kituo cha Buguruni.
Mashuhuda wanasema walipofungua mlango waliona mwili wa marehemu ukiwa umelala kitandani kwa takribani siku tano.
Kamishina Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Ilala, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho.
“Taarifa walizipata kutoka kwa majirani, baada ya kupita siku tatu bila kumuona na kusikia harufu kali ikitoka chumbani mwake na ndipo walipoamua kuvunja mlango.
“Mwili wake ulikutwa umelala kifudifudi kitandani kwake ukiwa umeharibika tayari, majirani wanasema waliamua kuuvunja mlango baada ya kutomuona kwa siku tatu, lakini pia kusikia harufu iliyokuwa ikitokea chumbani mwake na wanasema marehemu alikuwa na ugonjwa wa kifafa,” amesema ACP Magomi.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi na unatarajiwa kusafirishwa leo Januari 28, 2020 kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kwa ajili ya mazishi.
Enzi za uhai wake marhemu aliwahi kufanya kazi katika vyombo vya habari vya DARMPYA BLOG & TV ONLINE, LEMUTUZ BLOG & TV ONLINE na mpaka kifo kinamkuta alikuwa anafanya kazi kwa kujitolea katika Kituo cha TBC ONLINE.

