Tanzia: RC Mstaafu wa Dar Mama Mary Chips Afariki Dunia

Familia ya Chipungahelo na Zayumba inasikitika kutangaza kifo cha mama yao mpendwa Mary Alice Chipungahelo (Mama Chipps) kilichotokea tarehe 09/05/2021 majira ya saa 8 mchana katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar Es Salaam.

 

Msiba uko Magomeni Mapipa Mtaa wa Takadiri kwa Mama Joyce Nkondola.

 

Taarifa zaidi za ratiba ya mazishi zitatolewe baadae.

 

TAHADHARI: Familia Inaomba Tuchukue Tahadhari Kwa Kuvaa BARAKOA Kwenye Mikusanyo.

 

MFAHAMU ZAIDI KUHUSU MAMA CHIPS

Huyu ni mama wa familia, kiongozi mstaafu na mwalimu kitaaluma. Kabla ya kuingia katika siasa alifanya kazi ya ualimu, ikiwamo kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru mwaka 1953-1959.

 

Mbali na ualimu, Mama Chips aliwahi kufanya kazi katika Idara ya Elimu ya Watu Wazima, kuongoza Chuo cha Maendeleo ya Wanawake Vijijini cha Rungemba, Mkuu wa wilaya, katibu wa CCM, Katibu wa UWT, Mkuu wa Mkoa na kamu balozi.

 

Atakumbukwa kwa ujasiri wake pale alipomkabili na ‘kumdhibiti’ aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa enzi zile, Augustino Mrema aliyonekana kuingilia utendaji kazi wake, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini yeye akamwambia wazi asimwingilie.

 

Mrema wakati huo alikuwa amejijengea umaarufu kutokana na staili ya utendaji wake wa kupambana na uhalifu enzi za Utawala wa Awamu ya Pili, chini ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, hadi akapewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu nje ya Katiba.

 

Mama Chips kama anavyofahamika, alimweleza bayana Mrema, “kama kweli nia yako ni kufanya kazi, basi ukafanye kazi katika mikoani mingine na si Dar es Salaam ambako mimi ni mkuu wake.”

 

Hata hivyo, mkwara wake huo haukudumu: Siku chache baadaye aliondolewa kwenye nafasi hiyo, na huo ukawa ndio mwanzo wa kuachana na siasa mwaka 1993, akiwa amedumu katika nafasi hiyo kwa miaka minne akitokea mkoani Iringa alipokuwa Katibu wa CCM.

 

Shughuli baada ya kustaafu

Baada ya kuongoza Mkoa wa Dar es salaam, Mama Chips aliteuliwa kwenda Canada kuwa Kaimu Balozi wa Tanzania nchini humo, kazi aliyoifanya mpaka mwaka 1997 aliporejea nchini na kuendelea na shughuli binafsi.

 

Aliporudi nchini alijishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji wa kuku kwa muda mrefu…. baadaye alidilisha biashara na kufungua Kituo cha Kulea Watoto (Day Care Center).

 

Mama Chips aliyekataa katakata kutaja umri wake, alipata elimu ya sekondani Machame mwaka 1947-1950 na baadaye kupata mafunzo mafunzo ya ualimu katika 1951-1952. Pia alipata mafunzo ya Siasa katika chuo cha kivukoni na kozi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

 

 Tecno


Toa comment