The House of Favourite Newspapers

TAPELI MREMBO WA NITUMIE KWA NAMBA HII ANASWA

MOROGORO: Mrembo mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, amenaswa katika tukio la utapeli wa fedha za mtandao. 

 

Tukio hilo lililofunga umati wa watu lilitokea hivi karibuni katika mtaa wa Shamba Masika, katikati ya mji wa Morogoro kwenye duka la wakala wa fedha za mtandao, Upendo lsmail.

 

Awali, mwanahabari wetu alitonywa kuwepo kwa tukio hilo ambapo alifika fasta na kukuta umati wa watu ukiwa umemzunguka dada huyo wakisubiri polisi wafike. Hata hivyo, wakati mwanahabari wetu anaanza kupiga picha za tukio, askari walifika na kumzuia asitimize majukumu yake.

 

Wananchi wenye hasira walipoona tukio hilo, waliingilia kati kwa kuwavaa polisi na kuwataka kumuacha mwanahabari wetu aendelee na majukumu yake. Baada ya mwanahabari wetu kuzongwa sana na polisi hao kisha wananchi kuingilia kati, alipata nafasi ya kupiga picha kadhaa za tukio kisha kuzungumza na wakala huyo wa fedha za mtandao.

“Huyu dada alikuja akaomba nimtumie shilingi laki tano kwa njia ya mtandao wa simu cha ajabu baada ya kutuma pesa hiyo akadai kawasiliana na ndugu yake eti pesa haijafika, tukaanza kuzozana, nikamtega nikamwambia nipe hiyo laki tano (cash) nitume tena, hakuwa nayo. Nikamwitia mwizi watu wakamkong’ota badaye tukamfungia ndani tukaita polisi ndio wakafika,” alisema wakala huyo.

 

Wakala huyo alisema, baada ya vurugu hizo kutulia, polisi walimchukua yule dada aliyedaiwa kuwa tapeli pamoja na yeye, wakaelekea Kituo Kikuu cha Polisi. “Kwa kuwa polisi walikuja na gari dogo waliniambia mimi nipande bodaboda tulipofika wakamsweka ndani nikatoa maelezo, wakanipa namba ya kesi MOR/RB/7902/19 WIZI WA MTANDAO.

“Kesho Jumatano (jana) tunaenda mahakamani,” alisema Pendo. Wakizungumza na Amani, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo kwa sharti la kutotaja majina yao, waliliomba jeshi la polisi kufanya kazi kwa weledi na kutozuia wanahabari kutimiza majukumu yao.

 

“Hii sio mara ya kwanza naona tukio kama hili tena kwa mwandishi huyuhuyu hapa Morogoro, hawa polisi wajirekebishe, wafanye kazi yao na wawaache waandishi wafanye kazi yao,” alisema mmoja wa shuhuda huku akiungwa mkono na wenzake.

 

Alipotafutwa ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa Morogoro, SACP Wilbroad Mutafungwa kuhusiana na tukio hilo, alikuwa ametoka na simu yake iliita bila kupokelewa.

Comments are closed.