The House of Favourite Newspapers

Tatizo la Fangasi Kwa Mjamzito, Nini Kinasababisha Kuugua? Soma Hapa

0

Wakati wa ujauzito wanawake wengi hupata hofu juu ya kushika maambukizi yoyote kwani yanaweza kuathiri ukuaji wa mtoto tumboni.

 

Fangasi ukeni kwa mjamzito ni moja ya maambukizi kwenye uke yanawatokea sana wajawazito. Kutokana na mabadiliko ya homoni na mazingira ya ukeni, wengi wanaugua zaidi fangasi.

 

NINI KINASABABISHA MJAMZITO KUUGUA FANGASI?

Fangasi ukeni huletekezwa na kimelea wanaoitwa Candida. Fangasi aina ya candida wanapatikana katika maeneo mengi ya mwili ikiwemo ukeni , kwenye ngozi na njia ya haja kubwa. Katika hali ya kawaida ya mwili hawana madhara kabisa mpaka pale kinga yako itakaposhuka au mazingira ya eneo husika kubadilika ndipo utaanza kuugua.

 

Wajawazito wanaugua sana fangasi kutokana na mabadiliko ya homoni kutokana na mimba. Wakati wa ujauzito, kinga ya mwili hubadilika, homoni kama estrogen na progesterone kuongezeka zaidi.Vyote hivi vinachangia kwa fangasi ukeni kukua kupita kiasi na kuleta madhara.

 

DALILI

Dalili kubwa za fangasi ukeni kwa mjamzito ni; muwasho ndani ya uke na kwenye mashavu ya uke, kutokwa na uchafu mweupe kama maziwa mtindi, maumivu na hali ya kuungua ukeni, maumivu makali wakati wa tendo la ndoa na kupata harufu mbaya ukeni.

JE KUNA MADHARA YOYOTE YA FANGASI KWA MTOTO ALIYE TUMBONI?

Kwa kiasi kikubwa hakuna madhara kwa mtoto kutokana na mjamzito kuugua fangasi.

Japo inaweza kutokea kama mama hajapona fangasi wakati wa kujifungua akamuambukiza mtoto.

 

UNAWEZAJE KUJIKINGA USIUGUE FANGASI ZA UKENI?

Fanya usafi vizuri wa uke wako mara kwa mara, epuka matumizi ya sabuni au manukato ukeni, vaa nguo ya ndani yenye matirio ya pamba ili kupitisha hewa na upunguze matumizi ya vyakula vya sukari kwani vinapunguza kinga na kukufanya uugue fangasi kiurahisi.

 

VIPIMO VYA FANGASI ZA UKENI KWA MJAMZITO

Hospitali daktari atakuuliza kuhusu dalili unazopata, baada ya hapo atachukua sampuli kidogo ya uchafu unaopata na kuupeleka maabara kwa ajili ya vipimo.

Daktari pia anaweza kuotesha uchafu wako (culture) ili kubaini aina ya fangasi wa candida wanaokusumbua.

 

MATIBABU YA HOSPITALI YA FANGASI UKENI KWA MJAMZITO

Kwa kiasi kikubwa fangasi za ukeni hutibika kirahisi sana kupitia dawa za kupaka au za kuingiza ukeni (antifungal cream & suppository).

Dawa hizi zitakupa nafuu ndani ya siku saba. Kwa mjamzito hakikisha kwanza unamwona daktari kabla ya kuanza kutumia dawa.

Daktari atakupima na kukupa uhakika kama kweli una fangasi au una maambukizi mengine.

 

TIBA ZA NYUMBANI KWA FANGASI ZA UKENI

Maziwa mtindi; maziwa mtindi ni tiba nzuri ya nyumbani kwa ajili ya tatizo la fangasi ukeni. Maziwa mtindi yana bakteria wazuri wanaoitwa lactobacillus acidophilus. Bakteria hawa ni muhimu katika kuimarisha kinga ya mwili kwenye uke wako na watakusaidia kuzuia ukuaji wa fangasi ukeni.

 

Chovya kiasi kidogo cha maziwa, weka ukeni kila siku. Hakikisha pia unakunywa glasi tatu za mtindi wa asili kila siku. Maziwa yako yasiongezewe sukari wala kemikali yoyote mbaya.

 

Mafuta ya nazi; ili kutibu fangasi za ukeni hakikisha unanunua mafuta asili ya nazi (virgin, cold pressed) ambayo hayajaongezewa kemikali zozote na pia yaliyokamuliwa pasipo kupitishwa kwenye moto mkali.

 

Pakaa kiasi kidogo cha mafuta ukeni mara mbili kwa siku asubuhi na jioni pia.

 

Apple cider vinegar: hii ni moja ya tiba asili maarufu sana kwa ajili ya fangasi za ukeni. Vinegar ya apple ikitumika vizuri inasaidia kuimarisha ukuaji wa bakteria wazuri kwenye uke wako.

 

Ili kupata faida zake vizuri hakikisha unanunua vinegar ya apple yenye sifa hizi (organic, unfiltered with the mother). Baada ya hapo chukua vinegar ujazo wa robo kikombe cha chai changanya na maji lita moja osha uke wako mara mbili kwa siku.

 

MUHIMU

Kwa mjamzito dawa za hospitali za kumeza ili kutibu fangasi hazitakufaa kwani zinaweza kusababisha mimba kuharibika na matatizo kwa mtoto endapo atazaliwa. Dawa za kupaka ukeni ni salama zaidi kwa mjamzito endapo umejaribu hizi tiba asili bila mafanikio.

NA DK. Chale, SIMU: +255 713 350 084

Leave A Reply