Tatizo la fangasi sehemu za siri kwa wanawake

K ATI ya maambukizi yanayowasumbua wanawake wengi duniani ni maambukizi ya fangasi sehemu za siri. Inakisiwa asilimia 75 ya wanawake wote duniani hupata maambukizi haya.  Maambukizi ya fangasi katika sehemu za siri za mwanamke husababishwa na uwepo wa fangasi wanaojulikana kitaalamu kama Candida albicans. Fangasi hupatikana kama vimelea vya kawaida katika mdomo, mpira wa kupitisha chakula sehemu inayojulikana kama pharynx, katika kibofu cha mkojo, uume na hata kwenye uke.

Mfumo mzuri wa kinga wa mwili pamoja aina fulani za bakteria wanaoishi pamoja na fangasi hawa husaidia sana katika kudhibiti maambukizi yanayosababishwa na aina hii ya fangasi.

Kwa kawaida, Candida albicans huishi kwenye uke na sehemu nyingine (kama zilivyoelezewa hapo juu) bila kusababisha madhara yoyote yale isipokuwa pale mazingira ya eneo husika yanapobadilika kama vile mabadiliko katika hali ya pH ya eneo husika (ifahamike ya kwamba pH ya kawaida ndani ya uke ni 4.0 – 4.5) au uwiano wake na vimelea wengine unapoharibiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya madawa aina ya antibiotics, kupungua kwa kinga mwilini kutokana na magonjwa mbalimbali n.k.

Maambukizi haya ya fangasi yanaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili; Maambukizi yasiyo makali ambapo katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi mara moja hadi nne kwa mwaka na dalili zake huwa si mbaya sana na maambukizi haya husababishwa na fangasi wa jamii hii ya Candida albicans.

Pili maambukizi makali yaani complicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne kwa mwaka, dalili zake kuwa mbaya zaidi au kama maambukizi yatakuwa yametokea kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari, upungufu wa kinga mwilini. Aina hii husababishwa na vimelea vya aina nyingine tofauti na Candida albicans.

Wanawake walio katika hatari ya kupata maambukizi ya fangasi hawa ni wale wenye kutumia sana dawa aina ya detergents kwenye sehemu za siri au douches (vifaa vinavyotumiwa kusafishia uke kwa kutumia maji yaliyochanganywa na siki au antiseptic yoyote ile) kwa sababu husababisha kuharibika kwa uwiano wa fangasi na aina nyingine ya vinyemelezi kama bakteria aina ya lactobacilli

Au kutumia sana madawa aina ya antibiotics, steroids ambayo yana tabia ya kushusha kinga ya mwili ama kuwa na mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini ambayo husababisha mabadiliko katika sehemu za siri na hivyo kufanya kuwepo kwa ukuaji wa kasi wa fangasi hawa.

Lakini pia ujauzito husababisha fangasi hawa kuwa wengi sehemu nyeti kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na kupungua kwa kinga ya mwili. Hata hivyo ieleweke hapa kuwa si kila mjamzito hupatwa na maambukizi haya.

Matumizi ya dawa za kupanga uzazi (vidonge vya majira), upungufu wa kinga mwilini kutokana na magonjwa sugu kama kisukari, saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya mononucleosis na nk., ugonjwa wa ukimwi (HIV/AIDS, matibabu ya homon (hormonal replacement therapy) kutokana na sababu mbalimbali, matibabu ya kusaidia kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazi, msongo wa mawazo (stress) na utapia mlo (malnutrition) husababisha fangasi hawa sehemu za siri.

Lakini pia kuvaa nguo au mavazi yanayoleta joto sana sehemu za siri kwa muda mrefu kama nguo za kuogelea (swimwear), nguo za ndani (chupi) zilizotengenezwa kwa kitambaa aina ya nylon, nguo za ndani zinazobana sana nk, kujamiana kwa njia ya kawaida mara tu baada ya kujamiana kupitia njia ya haja kubwa au matumizi ya vilainishi venye glycerin wakati wa kujamiana.

Wanawake wenye umri wa miaka kati ya ishirini na thelathini wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya ya fangasi sehemu za siri wakati wale ambao wameshaacha kupata hedhi au wale ambao hawajaanza kupata hedhi kabisa hawako kwenye hatari kubwa.

Wiki ijayo tutaeleza dalili, tiba yake na viashiria, usikose nakala ya gazeti hili uelimike.


Loading...

Toa comment