The House of Favourite Newspapers

TATIZO LA FANGASI SEHEMU ZA SIRI LINAVYOWATESA WENGI!

KATI ya maambukizi yanayowasumbua wanawake wengi duniani ni maambukizi ya fangasi sehemu za siri ambayo husababishwa na uwepo wa fangasi wanaojulikana kitaalamu kama Candida albicans.  

 

Fangasi hawa hupatikana kama vimelea vya kawaida katika mdomo, mpira wa kupitisha chakula sehemu inayojulikana kama pharynx, katika kibofu cha mkojo, sehemu za siri za mwanaume na za mwanamke. Mfumo mzuri wa kinga wa mwili pamoja aina fulani za bakteria wanaoishi pamoja na fangasi hawa husaidia sana katika kudhibiti maambukizi yanayosababishwa na aina hii ya fangasi.

 

Kwa kawaida, Candida albicans huishi sehemu ya siri ya mwanamke na sehemu nyingine kama zilivyoelezewa hapo juu bila kusababisha madhara yoyote yale isipokuwa pale mazingira ya eneo husika yanapobadilika au uwiano wake na vimelea (microorganisms) wengine unapoharibiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya madawa aina ya antibiotics, kupungua kwa kinga mwilini kutokana na magonjwa mbalimbali n.k.

Maambukizi haya ya fangasi yanaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili, moja; Maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi mara moja hadi nne kwa mwaka na dalili zake huwa si mbaya sana na maambukizi haya husababishwa na fangasi wa jamii hii ya Candida albicans.

 

Pili, maambukizi makali yaani complicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne kwa mwaka, dalili zake kuwa mbaya zaidi au kama maambukizi yatakuwa yametokea kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari, upungufu wa kinga mwilini. Aina hii husababishwa na vimelea vya aina nyingine tofauti na Candida albicans.

 

Watu walio katika hatari ya kupata maambukizi ya fangasi hawa ni wale wenye kutumia sana dawa aina ya detergents kwenye sehemu za siri au douches (vifaa vinavyotumiwa kusafishia uke kwa kutumia maji yaliyochanganywa na siki au antiseptic yoyote ile) kwa sababu hali husababisha kuharibika kwa uwiano wa fangasi na aina nyingine ya vinyemelezi kama bakteria aina ya lactobacilli.

 

Pia watu wanaotumia sana madawa aina ya antibiotics, steroids ambayo yana tabia ya kushusha kinga ya mwili husababisha fangasi kuwepo eneo hilo, pia mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini ambayo husababisha mabadiliko katika sehemu za siri na hivyo kufanya kuwepo kwa ukuaji wa kasi wa fangasi hawa.

Wengine wanaougua sana fangasi sehemu za siri ni wenye ujauzito (kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na kupungua kwa kinga ya mwili). Hata hivyo ieleweke hapa kuwa si kila mjamzito hupatwa na maambukizi haya.

 

Pia matumizi ya dawa za kupanga uzazi (vidonge vya majira na upungufu wa kinga mwilini kutokana na magonjwa sugu kama kisukari, saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya mononucleosis husababisha tatizo hili. Pia ugonjwa wa Ukimwi (HIV/AIDS) na matibabu ya homoni (hormonal replacement therapy) kutokana na sababu mbalimbali na matibabu ya kusaidia kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazihupata maambukizi.

Makala haya yataendelea  wiki ijayo. Usikose!

Comments are closed.