The House of Favourite Newspapers

TATIZO LA KUKOSA HEDHI (AMENORRHEA)

KWA kawaida, mtoto wa kike akishafikia umri wa kuvunja ungo, anaanza kuona siku zake za hedhi. Huendelea kuona siku zake kwa kipindi chote cha maisha yake, mpaka anapofikia umri wa ukomo wa hedhi.  

 

Siku pekee ambazo mwanamke hatakuwa akiona siku zake, ni pale anapokuwa mjamzito mpaka miezi kadhaa baada ya kujifungua.

Hata hivyo, wapo ambao licha ya kufikisha umri wa kuvunja hedhi, huwa hawazioni siku zao na tatizo hili huweza kuendelea kwa kipindi kirefu na kumsababishia mhusika matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na kukosa uwezo wa kunasa ujauzito. Tatizo hili kitaalamu huitwa Amenorrhea.

 

Tatizo hili limekuwa likiwaletea usumbufu mwingi wa kisaikolojia wanawake wengi waliowahi kukumbana nalo. Tatizo hili limegawanyika katika makundi mawili: primary amenorrhea na seconday amenorrhea.

 

PRIMARY AMENORRHEA

Hii ni hali ya kukosa hedhi inayoweza kumtokea msichana aliye katika umri wa kuvunja ungo na ambayo huweza kuendana na hali ya kukosa mabadiliko ya kuvunja ungo kama vile kutoota matiti au kutoota nywele za sehemu za siri au msichana anaweza kuwa na mabadiliko ya kuvunja ungo lakini asipate hedhi.

 

SECONDARY AMENORRHEA

Hali hii humtokea mwanamke ambaye si mjamzito, hanyonyeshi na ambaye hajavuka umri wa kukosa hedhi (menopause) na wala hatumii njia za kisasa za uzazi wa mpango na ambaye hapo awali alikuwa akipata hedhi kama kawaida lakini akasimama kwa miezi mitatu au zaidi bila sababu yoyote inayojulikana.

 

SABABU ZA TATIZO

Zipo sababu au matatizo mengi yanayoweza kusababisha mwanamke akakosa hedhi japokuwa si mjamzito.

Matatizo hayo ni pamoja na:

-Mwanamke au msichana kuzaliwa na dosari kwenye uke, shingo ya uzazi au mji wa mimba (uterus).

-Kuta za uterus zinazotazamana kujishikiza pamoja.

-Utando unaozunguka uke (hymen) kuziba kabisa na kukosekana kwa tundu la kupitishia damu ya hedhi (imperforate hymen).

 

-Kuwepo kwa utando unaokatiza katika uke unaozuia damu ya hedhi kushindwa kutoka.

Pia sababu nyingine ni mabadiliko katika mwili wa mwanamke. Mabadiliko yanayoweza kuathiri mwili wa mwanamke na kumfanya ashindwe kupata hedhi ni pamoja na:

-Kula kiasi kidogo sana cha chakula kuliko kawaida au kula kupita kiasi.

-Unene uliopitiliza au kupungua uzito/kukonda isivyo kawaida.

-Uwepo wa magonjwa sugu kama vile kifua kikuu na utapiamlo.

 

-Msongo wa mawazo na matumizi ya madawa ya kulevya.

-Matumizi ya baadhi ya madawa hususan baadhi ya dawa za kutibu magonjwa ya akili.

-Kuwa na hofu iliyopitiliza.

-Kufanya mazoezi ya mwili kupita kiasi.

DALILI ZA TATIZO

Kukosa hedhi siyo ugonjwa bali ni dalili ya kuwepo kwa tatizo au ugonjwa fulani katika mwili. Kulingana na ugonjwa unaosababisha tatizo hili, kukosa hedhi kunaweza kuambatana pia na:

-Matiti kutoa maziwa wakati mwanamke si mjamzito na wala hanyonyeshi, maumivu ya kichwa na matatizo katika kuona vitu ambavyo kwa pamoja vinaweza kuashiria uwepo wa uvimbe katika ubongo.

-Mwanamke kuwa na nywele na vinyweleo vingi mwilini na kuota ndevu kama mwanaume, hali inayoashiria kuwepo kwa wingi kwa homoni za kiume za Androgen.

 

-Ukavu katika uke, kutoka jasho sana wakati wa usiku, au mabadiliko katika kupata usingizi vinaweza kuashiria matatizo katika Ovary.

-Kuongezeka uzito kupita kiasi au kupungua kwa uzito isivyo kawaida.

-Mwanamke kuwa na mhemko kuliko kawaida yaweza kuashiria kuwepo kwa matatizo ya kiakili na kisaikolojia.

 

UCHUNGUZI NA VIPIMO

Msichana yeyote aliyefikia umri wa kuvunja ungo na ambaye bado hajaanza kupata mabadiliko yeyote ya kubalehe katika mwili wake, hana budi kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Aidha msichana aliyefikia umri wa miaka 16 na ambaye bado hajaanza kupata hedhi anatakiwa pia kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

 

Kwa wanawake waliokuwa wakipata hedhi kama kawaida lakini ghafla wakaacha kupata kwa muda wa miezi mitatu mfululizo au zaidi nao pia hawana budi kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo hili. Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanywa kuchunguza sababu za kukosa hedhi kwa mwanamke:

Comments are closed.