TATIZO LA KUKOSA HEDHI WAKATI SI MJAMZITO (AMENORRHEA)

KWA kawaida, mtoto wa kike akishafikia umri wa kuvunja ungo, anaanza kuona siku zake za hedhi. Huendelea kuona siku zake kwa kipindi chote cha maisha yake, mpaka anapofikia umri wa ukomo wa hedhi.  Siku pekee ambazo mwanamke hatakuwa akiona siku zake, ni pale anapokuwa mjamzito mpaka miezi kadhaa baada ya kujifungua.

Hata hivyo, wapo ambao licha ya kufikisha umri wa kuvunja hedhi, huwa hawazioni siku zao na tatizo hili huweza kuendelea kwa kipindi kirefu na kumsababishia mhusika matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na kukosa uwezo wa kunasa ujauzito. Tatizo hili kitaalamu huitwa Amenorrhea. Zipo sababu au matatizo mengi yanayoweza kusababisha mwanamke akakosa hedhi japokuwa si mjamzito.

Matatizo hayo ni pamoja na:

-Mwanamke au msichana kuzaliwa na dosari kwenye uke, shingo ya uzazi au mji wa mimba (uterus).

-Kuta za uterus zinazotazamana kujishikiza pamoja.

-Utando unaozunguka uke (hymen) kuziba kabisa na kukosekana kwa tundu la kupitishia damu ya hedhi (imperforate hymen).

-Kuwepo kwa utando unaokatiza katika uke unaozuia damu ya hedhi kushindwa kutoka.

Pia sababu nyingine ni mabadiliko katika mwili wa mwanamke. Mabadiliko yanayoweza kuathiri mwili wa mwanamke na kumfanya ashindwe kupata hedhi ni pamoja na:

-Kula kiasi kidogo sana cha chakula kuliko kawaida au kula kupita kiasi.

-Unene uliopitiliza au kupungua uzito/kukonda isivyo kawaida.

-Uwepo wa magonjwa sugu kama vile kifua kikuu

na utapiamlo.

-Msongo wa mawazo na matumizi ya madawa ya kulevya.

-Matumizi ya baadhi ya madawa hususan baadhi ya dawa za kutibu magonjwa ya akili.

-Kuwa na hofu iliyopitiliza.

-Kufanya mazoezi ya mwili kupita kiasi.

DALILI ZA TATIZO

Kukosa hedhi siyo ugonjwa bali ni dalili ya kuwepo kwa tatizo au ugonjwa fulani katika mwili. Kulingana na ugonjwa unaosababisha tatizo hili, kukosa hedhi kunaweza kuambatana pia na:

-Matiti kutoa maziwa wakati mwanamke si mjamzito na wala hanyonyeshi, maumivu ya kichwa na matatizo katika kuona vitu ambavyo kwa pamoja vinaweza kuashiria uwepo wa uvimbe katika ubongo.

-Mwanamke kuwa na nywele

na vinyweleo vingi mwilini na kuota ndevu kama mwanaume, hali inayoashiria kuwepo kwa wingi kwa homoni za kiume za Androgen.

-Ukavu katika uke, kutoka jasho sana wakati wa usiku, au mabadiliko katika kupata usingizi vinaweza kuashiria matatizo katika Ovary.

Kuongezeka uzito kupita kiasi au kupungua kwa uzito isivyo kawaida.

-Mwanamke kuwa na mhemko kuliko kawaida yaweza kuashiria kuwepo kwa matatizo ya kiakili na kisaikolojia.

Itaendelea wiki ijayo

Toa comment