The House of Favourite Newspapers

TATIZO LA KUTOSHIKA MIMBA

TATIZO la kutoshika ujauzito, linasababisha matatizo makubwa bainaya wanandoa na upo ushahidi kwamba ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya tatizo hili ambalo kitaalamu huitwa infertility.  Wakati jamii ikiliona tatizo hili kuwa ni la mwanamke pekee, tafiti za kitaalamu zinaonesha kwamba mwanaume na mwanamke wote wanao uwezekano sawa wa kuwa na tatizo hili.

Kwa lugha nyepesi, inapotokea wanandoa wakashindwa kupata mtoto, inawezekana baba ndiyo akawa na tatizo na inawezekana mama ndiyo akawa na tatizo ingawa jamii yetu hutafsiri haraka kwamba mwanamke pekee ndiye mwenye matatizo. Kwa kuzingatia hilo, ni muhimu sana mume na mke kushirikiana mnapotafuta matibabu ya tatizo la mke kutoshika ujauzito. Badala ya kuanza kuhangaika kwa waganga wa kienyeji, inashauriwa kwamba wanandoa wanapaswa kuanza kwa kwenda hospitali.

Matibabu ya kutokushika mimba,kwanza kabisa daktari atatakiwa kuongea na wanandoa au watu wanaotaka mtoto kwani mara nyingi hukumbwa na matatizo ya kisaikolojia. Baada ya vipimo, daktari atawaeleza matatizo yao kwa kuyafafanua kwa kila mmoja, na kama kuna ugonjwa watajulishwa jinsi unavyoshambulia mwili.

Wataelezwa pia dalili za maradhi hayo na jinsi ya kuyatibu kama ni kwa njia ya vidonge au sindano au kwa upasuaji. Kwa wale wanene kupindukia (obesity) wataelekezwa jinsi ya kupunguza uzito bila madhara au kama wanatumia sigara au tumbaku na wanywaji wa pombe kupindukia, atawashauri kuacha mara moja.

Ikiwa watakuwa na tatizo la maumivu wakati wa tendo la ndoa au katikati ya mzunguko wa hedhi kwa wanawake, daktari atawapa dawa husika. Ili kupata mimba, wanandoa wanashauriwa kufanya tendo katikati ya siku za mzunguko, yaani kuanzia siku ya 12 hadi 16 baada ya hedhi.

Baadaye waende kwa daktari wakapime mkojo wa mama kwa kipimo cha kichocheo cha uzazi kijulikanacho kwa jina la Luteinizing Surge na kipimo kikionesha chanya (positive) basi wanandoa hao watatakiwa kukutana katika muda wa saa 24 hadi 36 baada ya majibu hayo ambayo huitwa kitaalamu LH Surge.

Kwa upande wa wanaume wenye matatizo ya kupungukiwa kwa mbegu za kiume yaani Oligospermia au hana mbegu kabisa au wenye kutoa kiasi kidogo cha ujazo na wale ambao hawawezi kusimamisha jogoo, watahitaji kumuona daktari na kupatiwa tiba.

USHAURI

Wanaume wanashauriwa kubadili njia ya maisha kwa kufanya mazoezi, kama walikuwa wanywaji wa pombe au wavutaji wa sigara au tumbaku, wanashauriwa kuacha mara moja. Watashauriwa pia kuacha kutumia dawa zinazoleta hitilafu katika utengenezaji wa mbegu za kiume. Dawa hizo ni kama vile Cimetidina, Nifedipine, dawa za mionzi au dawa zinazofanya kazi kwenye mfumo wa akili au za kuzuia degedege.

Comments are closed.