The House of Favourite Newspapers

Tatizo la mtoto wa jicho! (cataract)

MTOTO wa jicho kwa lugha nyingine huitwa cataract hutokana na kufanyika kwa ukungu katika lensi ya jicho. Mtu aliye na ukungu huu kuona kwake ni sawasawa na mtu anavyoona nje kupitia dirisha la kioo lenye ukungu wa barafu au maji dirishani wakati mvua inapokuwa inanyesha.

Ukungu huu hutokea na kuendelea kufunika jicho zima polepole kwa muda fulani na hatimaye mtu anashindwa kabisa kuona. Kwa mara ya kwanza, ukungu unapoendelea kutokea, mtu anaweza kupata miwani inayoweza kumsaidia kuona, lakini baada ya muda fulani kupita, mtu anaweza asione kabisa hadi afanyiwe matibabu mengine ya upasuaji.

Matibabu ya upasuaji ni salama, rahisi na yenye uhakika na ni ya muda mfupi, huchukua muda mfupi mgonjwa kupona na kurudia kazi zake za kawaida. Aina nyingi za ukungu machoni au mtoto wa jicho huwa ni tatizo linalotokea kama mabadiliko kwenye lensi ya jicho kadiri mtu anavyozeeka.

Baadhi ya watu hurithi hali ya kupata tatizo hili la ukungu kwenye macho na huwa hatarini kupata mapema zaidi.

Ukungu kwenye jicho unaweza kusababishwa na mambo mengine mengi kama magonjwa ya kisukari, jeraha au kufanyiwa upasuaji wa jicho. Madawa aina ya steroid pia husababisha kufanyika kwa ukungu kwenye lensi ya jicho.

Lensi (ambayo ukungu huu hutokea) huwa nyuma ya sehemu nyeusi ya jicho inayoonekana mtu akitazamwa kwenye jicho. Lensi hii hufanya kazi ya kuelekeza mwanga sehemu ya jicho inayoitwa retina ambapo hapa mwanga huo hubadilishwa na kufanywa kuwa umbo la kitu kama vile tunavyoona tukiangalia vitu vinavyotuzunguka.

Ukungu huu unapofanyika husababisha kutawanywa kwa miale ya mwanga hivyo haiingii kwenye retina, hatimaye mtu anaona ukungu na dalili nyingine zinazompata mwathirika wa tatizo hili. Mtu anapoendelea kuongezeka umri na kuzeeka, kuta za lensi huongezeka upana na kusababisha uwezo mdogo wa kupitisha mwanga.

Kwenye umri mkubwa pia, chembe hai za lensi huvunjika na kutuwama pamoja kutengeneza ukungu sehemu mojawapo ya ndani, ukungu unapoendelea kufanyika, basi mtu anapoteza hali ya kawaida ya kuona.

Ukungu kwenye jicho unaweza kutokea kwenye jicho moja tu, lakini mara nyingi hutokea kwenye macho yote. Mara nyingi pia si lazima macho yote yapatwe na dalili zinazofanana, hivyo ukungu kwenye jicho moja unaweza kuwa na dalili mbaya zaidi ya jicho lingine.

Mambo yafuatayo yanamuweka mtu hatarini kupata mtoto wa jicho; Kuongezeka umri (umri mkubwa yaani uzee), kisukari, kunywa pombe kupita kiwango, kupatwa mara nyingi na mionzi kama ya X-Ray au matibabu ya saratani kwa njia ya mionzi au kuwa na historia ya mtoto wa jicho kwenye familia.

Sababu nyingine ni kuwa na shinikizo la juu la damu, uzito kupita kiwango, kuumia jicho au michomo kwenye jicho, kufanyiwa upasuaji wa jicho au macho au matumizi ya muda mrefu ya dawa aina ya steroids na uvutaji wa sigara.

DALILI

Dalili za mtu mwenye mtoto wa jicho au ukungu kwenye jicho huwa ni kati ya hizi zifuatazo; kuona ukungu au vitu vimefifia, kupata shida kuona wakati wa usiku, kuumizwa macho kwa mwanga, kuona nusu duara au duara kwenye mwanga unaong’aa au miale ya mwanga kama vile upinde wa mvua unavyokaa.

Kubadilisha mara kwa mara kwa lensi ya miwani kutokana na hali ya macho kuwa mbaya. Kuona rangi zimefifia au rangi ya vitu kuwa njano, kuona kitu kimoja kwamba ni viwili katika jicho moja. Mwanzo wa tatizo hili la ukungu kwenye lensi ya jicho huweza kudhuru sehemu ndogo ya jicho kiasi kwamba hutapata dalili zozote, muda unapoendelea na ukungu huu kutanda kwenye sehemu kubwa ya lensi ya jicho, ndipo utakapoanza kupata dalili hizo.

Wakati gani uonane na daktari? Fanya mipango ya kuonana na daktari endapo unaona kuna mabadiliko yoyote katika macho yako kama kuona kitu kimoja kuwa mara mbili, kuona ukungu n.k.

Kupima kujua kama una mtoto wa jicho, daktari atafanya vipimo vifuatavyo;

Kukuomba usome chati yenye maandishi makubwa na madogo kuona kiwango chako cha kuona kitaalam huitwa visual acuity test. Jicho moja hufunikwa na baada ya kupimwa, hivyohivyo lingine hufunikwa na kupimwa kwa kutumia kifaa cha kamera na mwanga kuangalia jicho na lenzi ya jicho. Kifaa hiki kinajulikana kama microscopy, kutanua dirisha la jicho kwa ajili ya kuchunguza retina.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.