TCRA Yawakaanga Cable TV Kanda ya Ziwa

MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA) Kanda ya Ziwa imewapiga marufuku wamiliki wa Cable TV kuonyesha vipindi ambavyo havitakiwi katika cable zao ikiwemo michezo yote ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Laliga ikiwa ni matakwa ya sheria inayoongoza sekta hiyo.

 

Akizungumza na wamiliki wa Cable TV wa mikoa yote ya kanda hiyo, Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo, alisema (Cable TV Operators) hutoa huduma husika kwa mujibu wa sheria Na.7 ya Mwaka 1999 ya kanuni za Mawasiliano ya kietroniki na posta (miundombinu na huduma za utangazaji za kidijitali) za mwaka 2018  na masharti ya leseni yanaelekeza nini kwa wateja.

 

“Tumefanya mkutano huu ili kuweza kuondoa tofauti na mkanganyiko kwa watoa huduma wetu kati ya watu wanaotumia Cable TV na wale wa ving’amuzi ili kujua haki na mipaka ya kila mtoa huduma, ikiwa ni marufuku kuonyesha mipira ya Ligi Kuu ya Tanzania inayosimamiwa na shirikisho la soka (TFF), Ligi ya Uingereza na Hispania haionyeshwi kwa kutumia Cable, bila kujali anayapatia kupitia teknolojia gani,” alisema Mihayo.

Aliongeza kwamba watoa huduma wote wa maudhui kwa kutumia cable (Cable TV Operators) wahakikishe  kuwa wanaondoa chaneli za maudhui yaliyozuiliwa kwa mujibu wa sheria mpaka watakapowasilisha mikataba ya makubaliano, la sivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtoa huduma atakayekiuka sheria, kanuni, taratibu na masharti ya leseni yake kama ilivyoelekezwa.

 

“Sisi ni walezi wenu hivyo tulikubaliana kuwa tuanze kwa kukakaa kwanza kabla ya kuanza kufuatilia sheria na kanuni jinsi zinavyotaka ili siku tukianza tusilaumiane kwani tunafahaumu tangu mwanzo hakuna mahusiano mazuri kati ya watu wa cable na wa ving’amuzi hususani watu wa DStv kwani wamekuwa na malalamiko ya kudukuliwa kwa chaneli ambazo wana haki nazo kisheria,” alisisitiza.

Na Leah Marco, MWANZA

Toa comment