The House of Favourite Newspapers

TCRA Yawanasa Wanaodaiwa Kuiba Mamilioni Benki – Video

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewafikisha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu watu sita wakikabiliwa na mashtaka nane ikiwemo la kuisababishia hasara Serikali na TCRA ya sh.Mil.963.9.

 

Washitakiwa hao wamesomewa makosa yao na Wakili wa Serikali, Jacqline Nyantori mbele ya Hakimu Mkazi Vicky Mwaikambo. Miongoni mwa washtakiwa hao ni Yusuph Saninga, Michael Buholo, Rashid Midole,Eliud Patrick,Lameck Alute na Adam Kionga.

 

Katika Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 110/2019, wakili amedai kati ya Januari 1 na Septemba mwaka huu 2019 jijini Dar es Salaam washtakiwa walikula njama ya kufanya udanganyifu wa kimawasiliano.

 

Imeelezwa kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa Yusuph Saninga kinyume cha sheria aliingiza vifaa Vya mawasiliano nchini bila ya kuwa na leseni kutoka mamlaka ya mawasiliano Tanzania(TCRA).

 

Miongoni mwa vifaa hivyo ni Gateway modem E1 Transmitter aina ya Rad yenye serial namba 805000783 ASM1-52/E1/2W, Router Voice Over Internet Protocol (VOIP) Gateway serial namba 16M2RMVS19030788 yenye chaneli 16.

 

Katika kipindi hicho, washtakiwa hao wanadaiwa kufanya matumizi ya mawasiliano kulaghai kwa nia ya kukwepa maalipo halali ya serikali kwa kupokea na kusambaza mawasiliano bila ya kuwa na kibali cha TCRA.

 

Katika mashitaka hayo, Wakili Nyantori amedai Machi 29, mwaka huu katika Benki ya KCB tawi la Uhuru Ilala Dar es Salaam, mshtakiwa Saninga alihamisha dola za kimarekani 4,740 sawa na Sh 11,298,863.98 kupitia Western Union kwa Liwen Si, Mkazi wa Shenzhen China kwa lengo la kuficha chimbuko la kihalifu wakati akijua ni zao la kosa la kutumia kulaghai mawasiliano.

 

Katika shtaka la kusababisha hasara, inadaiwa kati ya Januari 11 na Septemba 15,2019 washtakiwa Saninga, Michael, Rashid, Eliud,Lameck na Adam wakijua kwa matendo yao na makusudi waliisababishia serikali na TCRA hasara ya Sh 963,585,000.

 

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mwaikambo aliwaeleza washtakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza Kesi hiyo.

 

Wakili Nyantori alieleza kuwa upelelezi wa Kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa. Washtakiwa walipelekwa rumande na kesi imeahirishwa hadi Oktoba 24, mwaka huu.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Global Publishers (@globalpublishers) on

Comments are closed.