The House of Favourite Newspapers
gunners X

Tenga Aeleza Umuhimu wa Ubia Sekta ya Umma na Binafsi

0

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria waPPP Centre, Flora Tenga, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha Ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) kama chachu ya kuvutia uwekezaji na kukuza viwanda vinavyoongeza pato la Taifa.

Tenga ameeleza hayo wakati wa Majadiliano ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Dialogue) kati ya Confederation of Tanzania Industries (CTI) na wazalishaji wa Mkoa wa Pwani, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki (Novemba 27, 2025), katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Katika mdahalo huo, Tenga amesema sekta ya viwanda ni nguzo muhimu katika maendeleo ya uchumi wa nchi, na ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, ni muhimu kuwa na mfumo imara wa PPP.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi utaharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa inayohitaji rasilimali na utaalamu wa pande zote mbili, hivyo kutoa fursa ya kukuza sekta ya viwanda na kuongeza ajira.

“Ubia huu unatoa fursa kwa wawekezaji kutoka sekta binafsi kushirikiana na serikali katika miradi mikubwa, hasa kwenye maeneo yenye changamoto kubwa za miundombinu.

Hii ni njia bora ya kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda inakua na kuchangia katika uchumi wa Taifa,” alieleza Mkurugenzi Tenga.

Tenga ametumia fursa hiyo pia kuhimiza wabia kuungana na PPP katika kutekeleza miradi Express Way kati ya Kibaha-Chalinze na Chalinze-Morogoro na kusema mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa Mkoa wa Pwani kwa kuboresha miundombinu ya kibiashara na kuongeza uwekezaji katika mkoa huo.

Katika mdahalo huo, mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ambaye alimuakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Kunenge.

Vilevile, ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasri, Mkurugenzi wa CTI, na wadau kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali, kama TISEZA na STAMICO, pamoja na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Leave A Reply