TFF Mnataka Mwinyi Zahera Afanye Kazi Benki!

 

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred (kilia) na kushoto ni  Afisa habari wa TFF, Clifford Ndimbo.

MATOKEO ya mchezo wa kwanza wa kufuzu kwa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania na Burundi yana faida kubwa kwetu. Mara nyingi makocha wengi wamekuwa wakienda ugenini kutafuta sare ya mabao na siyo sare ya kutofungana kwa kuwa hii imekuwa ikiwasaidia kwenye mchezo ujao.

 

Stars wana nafasi kubwa zaidi kwa sasa ya kuweza kufuzu kwa hatua hiyo, lakini hawatakiwi kuitumia vibaya nafasi hiyo kwa kuwa inaweza kuyeyuka kama watashindwa kuelewa kuwa wanatakiwa kupambana kwenye mchezo huo.

Mashabiki pia wanatakiwa kuhakikisha wanawaunga mkono Stars kama ambavyo wamekuwa wakifanya huko nyuma. Mara nyingi kamati za kusaidia Stars zimekuwa zikiteuliwa mwishoni wakati timu inakaribia kufuzu kwenye michuano fulani, lakini kwangu naona kuwa zilikuwa vyema ziteuliwe mapema au mwanzoni kabisa wa michuano kama hapa.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera (katikati).

Kusubiri zikiwa zimebaki mechi mbili halafu ndiyo inateuliwa kamati hakuna tija kubwa sana kwa kuwa kazi inakuwa ngumu sana, lakini kama wangeteuliwa kuanzia sasa basi wanaweza kuanza kuhamasisha kuanzia sasa hadi mwisho wa michuano hii. Nikiachana na jambo hilo, kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwenye kanuni mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusu mavazi ya viongozi wa benchi la ufundi wakiwemo makocha.

 

Kila kanuni mara nyingi lazima iwe na sababu yake, juzi iliripotiwa kuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amefungiwa michezo mitatu kutokana na kutoa maneno ya lawama kwa waendeshaji wa ligi pia akapigwa faini ya shilingi laki tano kutokana na kuvaa pensi kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting.

 

Kanuni hii ya mavazi bado inachanganya kwa kuwa kwanza TFF hawajasema vizuri kocha anayetakiwa kuvaa nadhifu anatakiwa avae nini? Anatakiwa kuvaa shati, jeans, traki suti, au anatakiwa kuvaa jezi za timu yake, au apige suti nyeusi kabisa?

 

Kuna maswali mengi ambayo TFF walitakiwa wayajibu kabla hawajaanza kutoa adhabu. Ninachofahamu mimi, Zahera ni mwana michezo na wala siyo mfanyakazi wa benki, kuanza kumlazimisha leo avae suti sioni kama ni haki kwa kuwa kazi yake inamtaka kuvaa kiuanamichezo. Nakumbuka makocha wakubwa duniani akiwemo Alex Ferguson alikuwa anavaa pensi kwenye mechi.

Nakumbuka hivi karibuni makocha wa Taifa Stars akiwemo kocha mkuu walivaa pensi kwenye mechi, hawa wanasimamiwa na nani? Nafahamu kuwa ni TFF.

 

Kama mdhamini wa Yanga, leo akitengeneza jezi na bukta kwa ajili ya makocha na viongozi wengine wa benchi la ufundi TFF watawazuia kuvaa? Nafikiri Zahera hawezi kuwa mfanyakazi wa benki aingie kwenye mechi amevaa shati jeupe tai na suruali ya kitambaa akiwa amechomekea.

 

Ulaya unaweza kufanya vizuri kwa kuwa uwanja na mazingira yote ni rafiki, kuna usafi na hata ukisimama una uhakika kuwa upo sehemu salama. Jiulize leo Zahera anavaa shati jeupe anakwenda kwenye mechi Jamhuri halafu mvua imenyesha, au anakwenda Manungu kukiwa na vumbi atatokaje? Sheria hii inaweza kufanya kazi lakini haiwezi kufanya vizuri kama haitafafanua kuwa TFF wanataka nini, lazima iseme kuwa ni mavazi gani yanatakiwa kwa kuwa kumzuia kocha kuvaa traki suti ni kumtoa kwenye utamaduni wa kazi yake.

Mtazamo Wangu na  PHILLIP NKINI


Loading...

Toa comment