The House of Favourite Newspapers

TFF: Simba, Yanga tafuteni viwanja vyenu

0

baraka1

Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto.

Mohammed Mdose, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limezipa muda usiopungua miezi sita klabu zote za Ligi Kuu Bara zikiwemo Simba na Yanga ziwe zimekamilisha masharti ya kupewa leseni ikiwemo kuwa na viwanja vyao wenyewe.

TFF imeziambia klabu hizo baada ya agizo kutoka Shirikisho la Soka la Kimtaifa (Fifa), kwamba kila klabu ya ligi kuu lazima iwe na leseni ya kushiriki ligi na moja ya masharti ya kuipata leseni hiyo ni kuwa na uwanja wake maalumu kwa mazoezi na mechi.

Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, alisema kuwa ilitakiwa msimu huu klabu ambayo haikukidhi vigezo hivyo isishiriki ligi kuu lakini baada ya kuona nyingi zina upungufu ndipo wakapewa leseni za muda.

Alisema kuwa kati ya timu 16 za ligi kuu, Mtibwa Sugar na Azam pekee ndizo zilizotimiza vigezo hivyo, huku akisisitiza zingine zihakikishe zinakamilisha ndani ya miezi sita ijayo.

“Ili timu iweze kushiriki michuano ya kimataifa lazima iwe na leseni na haipatikani mpaka ukidhi vigezo vyote vilivyowekwa ikiwemo kuwa na uwanja wako, tumeangalia kati ya timu zote, Mtibwa na Azam tu ndizo zimekidhi kwa asilimia 95, lakini wengine wote bado tumewapa leseni za muda wa miezi sita na kuwataka wahakikishe kabla ya muda huo kuisha lazima wawe wamekamilisha kila kitu ili tuwape leseni za kudumu,” alisema Kizuguto.

Leave A Reply